Zaburi 32
Furaha Ya Msamaha
Zaburi ya Daudi. Funzo.
Heri mtu yule ambaye amesamehewa makosa yake,
ambaye dhambi zake zimefunikwa.
Heri mtu yule ambaye Bwana
hamhesabii dhambi,
na ambaye rohoni mwake
hamna udanganyifu.
 
Niliponyamaza, mifupa yangu ilichakaa
kwa kulia kwa maumivu makali mchana kutwa.
Usiku na mchana
mkono wako ulinilemea,
nguvu zangu zilinyonywa
kama vile katika joto la kiangazi.
Kisha nilikujulisha dhambi yangu
wala sikuficha uovu wangu.
Nilisema, “Nitaungama
makosa yangu kwa Bwana.”
Ndipo uliponisamehe
hatia ya dhambi yangu.
 
Kwa hiyo kila mtu mcha Mungu akuombe
wakati unapopatikana,
hakika maji makuu yatakapofurika
hayatamfikia yeye.
Wewe ndiwe mahali pangu pa kujificha,
utaniepusha na taabu
na kunizunguka kwa nyimbo za wokovu.
 
Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea;
nitakushauri na kukuangalia.
Usiwe kama farasi au nyumbu
wasio na akili,
ambao ni lazima waongozwe kwa lijamu na hatamu
la sivyo hawatakukaribia.
10 Mtu mwovu ana taabu nyingi,
bali upendo usio na kikomo wa Bwana
unamzunguka mtu anayemtumaini.
 
11 Shangilieni katika Bwana na mfurahi, enyi wenye haki!
Imbeni, nyote mlio wanyofu wa moyo!