Zaburi 49
Upumbavu Wa Kutegemea Mali
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya wana wa Kora.
Sikieni haya, enyi mataifa yote,
sikilizeni, ninyi wote mkaao dunia hii.
Wakubwa kwa wadogo,
matajiri na maskini pamoja:
Kinywa changu kitasema maneno ya hekima,
usemi wa moyo wangu utatoa ufahamu.
Nitatega sikio langu nisikilize mithali,
nitafafanua kitendawili kwa zeze:
 
Kwa nini niogope siku mbaya zinapokuja,
wakati wadanganyifu waovu wanaponizunguka,
wale wanaotegemea mali zao
na kujivunia utajiri wao mwingi?
Hakuna mwanadamu awaye yote
awezaye kuukomboa uhai wa mwingine,
au kumpa Mungu fidia kwa ajili yake.
Fidia ya uhai ni gharama kubwa,
hakuna malipo yoyote yanayotosha,
ili kwamba aishi milele
na asione uharibifu.
 
10 Wote wanaona kwamba watu wenye hekima hufa;
wajinga na wapumbavu vivyo hivyo huangamia
na kuwaachia wengine mali zao.
11 Makaburi yao yatabaki kuwa nyumba zao za milele,
makao yao vizazi vyote;
ingawa walikuwa na mashamba
na kuyaita kwa majina yao.
 
12 Lakini mwanadamu, licha ya utajiri wake, hadumu;
anafanana na mnyama aangamiaye.
 
13 Hii ndiyo hatima ya wale wanaojitumainia wenyewe,
pia ya wafuasi wao, waliothibitisha misemo yao.
14 Kama kondoo, wamewekewa kwenda kaburini,*
nacho kifo kitawala.
Wanyofu watawatawala asubuhi,
maumbile yao yataozea kaburini,
mbali na majumba yao makubwa ya fahari.
15 Lakini Mungu atakomboa uhai wangu na kaburi,
hakika atanichukua kwake.
 
16 Usitishwe mtu anapotajirika,
fahari ya nyumba yake inapoongezeka,
17 kwa maana hatachukua chochote atakapokufa,
fahari yake haitashuka pamoja naye.
18 Ingawa alipokuwa akiishi alijihesabu kuwa heri,
na wanadamu wanakusifu unapofanikiwa,
19 atajiunga na kizazi cha baba zake,
ambao hawataona kamwe nuru ya uzima.
 
20 Mwanadamu mwenye utajiri bila ufahamu
ni kama wanyama waangamiao.
* Zaburi 49:14 Kaburini hapa ina maana ya Sheol kwa Kiebrania, yaani Kuzimu. Zaburi 49:15 Au: nafsi.