Zaburi 52
Hukumu Ya Mungu
Kwa mwimbishaji. Utenzi wa Daudi. Baada ya Doegi, Mwedomu kumwendea Sauli na kumjulisha kuwa: “Daudi amekwenda nyumbani kwa Ahimeleki.”
Ewe jitu, mbona unajivunia ubaya?
Kwa nini unajivuna mchana kutwa,
wewe ambaye ni fedheha mbele za Mungu?
Ulimi wako hupanga mashauri mabaya ya maangamizi.
Ni kama wembe mkali, ninyi mfanyao hila.
Unapenda mabaya kuliko mema,
uongo kuliko kusema kweli.
Unapenda kila neno lenye kudhuru,
ewe ulimi wenye hila!
 
Hakika Mungu atakushusha chini
kwa maangamizi ya milele:
atakunyakua na kukuondoa kwa nguvu
kutoka hema yako,
atakungʼoa kutoka nchi ya walio hai.
Wenye haki wataona na kuogopa,
watamcheka, wakisema,
“Huyu ni yule mtu ambaye
hakumfanya Mungu kuwa ngome yake,
bali alitumainia wingi wa utajiri wake,
na akawa hodari kwa kuwaangamiza wengine!”
Neema Ya Mungu
Lakini mimi ni kama mti wa mzeituni
unaostawi katika nyumba ya Mungu,
nautegemea upendo wa Mungu usiokoma
milele na milele.
Nitakusifu milele kwa yale uliyoyatenda,
nitatumaini jina lako, kwa kuwa jina lako ni jema.
Nitakusifu mbele ya watakatifu wako.