Zaburi 64
Kuomba Ulinzi Dhidi Ya Maadui
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.
Ee Mungu, unisikie ninapoeleza lalamiko langu,
uyahifadhi maisha yangu kutokana na vitisho vya adui.
Unifiche kutokana na shauri la siri la waovu,
kutokana na zile kelele za kundi la watenda mabaya.
 
Wananoa ndimi zao kama panga
na kuelekeza maneno yao kama mishale ya kufisha.
Hurusha mishale kutoka kwenye mavizio kwa mtu asiye na hatia,
humrushia ghafula bila woga.
 
Kila mmoja humtia moyo mwenzake
katika mipango mibaya;
huzungumza juu ya kuficha mitego yao,
nao husema, “Ni nani ataiona?”
Hufanya shauri baya la dhuluma na kusema,
“Tumebuni mpango mkamilifu!”
Hakika nia na moyo wa mwanadamu vina hila.
 
Bali Mungu atawapiga kwa mishale,
nao ghafula wataangushwa.
Atageuza ndimi zao wenyewe dhidi yao
na kuwaleta kwenye maangamizi;
wote wawaonao watatikisa vichwa vyao
kwa dharau.
 
Wanadamu wote wataogopa,
watatangaza kazi za Mungu
na kutafakari yale aliyoyatenda.
10 Wenye haki na wafurahi katika Bwana,
na wakimbilie kwake;
wanyofu wote wa moyo na wamsifu yeye!