Zaburi 67
Mataifa Yahimizwa Kumsifu Mungu
Kwa mwimbishaji. Na ala za nyuzi za muziki. Zaburi. Wimbo.
Mungu aturehemu na kutubariki,
na kutuangazia nuru za uso wake,
ili njia zako zijulikane duniani,
wokovu wako katikati ya mataifa yote.
 
Ee Mungu, mataifa na wakusifu,
mataifa yote na wakusifu.
Mataifa yote wafurahi na kuimba kwa shangwe,
kwa kuwa unatawala watu kwa haki
na kuongoza mataifa ya dunia.
Ee Mungu, mataifa na wakusifu,
mataifa yote na wakusifu.
 
Ndipo nchi itatoa mazao yake,
naye Mungu, Mungu wetu, atatubariki.
Mungu atatubariki
na miisho yote ya dunia itamcha yeye.