Zaburi 70
Kuomba Msaada
(Zaburi 40:13-17)
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Maombi.
Ee Mungu, ufanye haraka kuniokoa;
Ee Bwana, njoo hima unisaidie.
Wale wanaotafuta kuuondoa uhai wangu,
waaibishwe na kufadhaishwa;
wote wanaotamani kuangamizwa kwangu,
warudishwe nyuma kwa aibu.
Wale waniambiao, “Aha! Aha!”
warudi nyuma kwa sababu ya aibu yao.
Lakini wote wakutafutao
washangilie na kukufurahia,
wale wapendao wokovu wako siku zote waseme,
“Mungu na atukuzwe!”
 
Lakini bado mimi ni maskini na mhitaji;
Ee Mungu, unijie haraka.
Wewe ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu;
Ee Bwana, usikawie.