KITABU CHA TATU
73
(Zaburi 73–89)
Haki Ya Mungu
Zaburi ya Asafu.
Hakika Mungu ni mwema kwa Israeli,
kwa wale ambao mioyo yao ni safi.
 
Bali kwangu mimi, miguu yangu ilikuwa karibu kuteleza;
nilikuwa karibu mguu wangu kuachia uliposimama.
Kwa maana niliwaonea wivu wenye kujivuna
nilipoona kufanikiwa kwa waovu.
 
Wao hawana taabu,*
miili yao ina afya na nguvu.
Hawapati shida zinazowataabisha watu wengine,
wala hawapati mapigo kama wanadamu wengine.
Kwa hiyo kiburi ni mkufu wao,
wamejivika jeuri.
Uovu hutoka katika mioyo yao iliyokufa ganzi,
majivuno maovu kutoka mioyoni mwao hauna kikomo.
Hudhihaki na kusema kwa ukorofi,
katika majivuno yao wanatishia kutesa.
Vinywa vyao huweka madai hata kwa mbingu,
nazo ndimi zao humiliki duniani.
10 Kwa hiyo watu wao huwageukia
na kunywa maji tele.
11 Wanasema, “Mungu awezaje kujua?
Je, Yeye Aliye Juu Sana anayo maarifa?”
 
12 Hivi ndivyo walivyo waovu:
siku zote hawajali,
wanaongezeka katika utajiri.
 
13 Hakika nimeuweka moyo wangu safi bure,
ni bure nimenawa mikono yangu nisiwe na hatia.
14 Mchana kutwa nimetaabika,
nimeadhibiwa kila asubuhi.
 
15 Kama ningesema, “Nitasema hivi,”
ningelikuwa nimewasaliti watoto wako.
16 Nilipojaribu kuelewa haya yote,
yalikuwa magumu kwangu kuelewa.
17 Mpaka nilipoingia patakatifu pa Mungu,
ndipo nilipotambua mwisho wao.
 
18 Hakika unawaweka mahali pa utelezi,
unawaangusha chini kwa uharibifu.
19 Tazama jinsi wanavyoangamizwa ghafula,
wanatoweshwa kabisa na vitisho!
20 Kama ndoto mtu aamkapo,
hivyo wakati uinukapo, Ee Bwana,
utawatowesha kama ndoto.
 
21 Wakati moyo wangu ulipohuzunishwa,
na roho yangu ilipotiwa uchungu,
22 nilikuwa mpumbavu na mjinga,
nilikuwa mnyama mkatili mbele yako.
 
23 Hata hivyo niko pamoja nawe siku zote,
umenishika mkono wangu wa kuume.
24 Unaniongoza kwa shauri lako,
hatimaye utaniingiza katika utukufu.
25 Nani niliye naye mbinguni ila wewe?
Dunia haina chochote ninachokitamani ila wewe.
26 Mwili na moyo wangu vyaweza kushindwa,
bali Mungu ni nguvu ya moyo wangu
na fungu langu milele.
 
27 Wale walio mbali nawe wataangamia,
unawaangamiza wote wasio waaminifu kwako.
28 Lakini kwangu mimi,
ni vyema kuwa karibu na Mungu.
Nimemfanya Bwana Mwenyezi kimbilio langu;
nami nitayasimulia matendo yako yote.
* Zaburi 73:4 Tafsiri nyingine zinasema: hawana maumivu katika kufa kwao. Zaburi 73:10 Au: na kupokea yote wasemayo.