Zaburi 80
Maombi Kwa Ajili Ya Kuponywa Kwa Taifa
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Yungiyungi za Agano.” Zaburi ya Asafu.
Ee Mchungaji wa Israeli tusikie,
wewe umwongozaye Yosefu kama kundi;
wewe uketiye katika kiti cha enzi
katikati ya makerubi, angaza
mbele ya Efraimu, Benyamini na Manase.
Uamshe nguvu zako,
uje utuokoe.
 
Ee Mungu, uturejeshe,
utuangazie uso wako,
ili tuweze kuokolewa.
 
Ee Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote,
hata lini hasira yako itawaka na kufoka moshi
dhidi ya maombi ya watu wako?
Umewalisha kwa mkate wa machozi,
umewafanya wanywe machozi bakuli tele.
Tumekuwa chanzo cha ugomvi kwa jirani zetu,
na adui zetu wanatudhihaki.
 
Ee Mungu Mwenye Nguvu Zote, uturejeshe;
utuangazie uso wako,
nasi tuweze kuokolewa.
 
Ulileta mzabibu kutoka Misri,
ukawafukuza mataifa, ukaupanda.
Uliandaa shamba kwa ajili yake,
mizizi ikawa imara, ukajaza nchi.
10 Milima ilifunikwa kwa kivuli chake,
matawi yake yakafunika mierezi mikubwa.
11 Matawi yake yalienea mpaka Baharini,*
machipukizi yake mpaka kwenye Mto.
 
12 Mbona umebomoa kuta zake
ili wote wapitao karibu
wazichume zabibu zake?
13 Nguruwe mwitu wanauharibu
na wanyama wa kondeni hujilisha humo.
14 Turudie, Ee Mungu Mwenye Nguvu Zote!
Tazama chini kutoka mbinguni na uone!
Linda mzabibu huu,
15 mche ulioupanda kwa mkono wako wa kuume,
mwana uliyemlea
kwa ajili yako mwenyewe.
 
16 Mzabibu wako umekatwa, umechomwa moto,
unapowakemea, watu wako huangamia.
17 Mkono wako na utulie juu ya mtu aliyeko mkono wako wa kuume,
mwana wa mtu uliyemlea kwa ajili yako mwenyewe.
18 Ndipo hatutakuacha tena,
utuhuishe, nasi tutaliitia jina lako.
 
19 Ee Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote, uturejeshe;
utuangazie uso wako,
ili tuweze kuokolewa.
* Zaburi 80:11 Huenda inamaanisha Bahari ya Mediterania. Zaburi 80:11 Yaani Mto Frati.