Zaburi 82
Maombi Kwa Ajili Ya Kutaka Haki
Zaburi ya Asafu.
Mungu anaongoza kusanyiko kuu,
anatoa hukumu miongoni mwa “miungu”:
 
“Hata lini utaendelea kuwatetea wasio haki
na kuonyesha upendeleo kwa waovu?
Teteeni wanyonge na yatima,
tunzeni haki za maskini na walioonewa.
Mwokoeni mnyonge na mhitaji,
wakomboeni kutoka mkononi mwa mwovu.
 
“Hawajui lolote, hawaelewi lolote.
Wanatembea gizani;
misingi yote ya dunia imetikisika.
 
“Nilisema, ‘Ninyi ni “miungu”;
ninyi nyote ni wana wa Aliye Juu Sana.’
Lakini mtakufa kama wanadamu wa kawaida;
mtaanguka kama mtawala mwingine yeyote.”
 
Ee Mungu, inuka uihukumu nchi,
kwa kuwa mataifa yote ni urithi wako.