20
Kutekwa Kwa Raba
(2 Samweli 12:26-31)
1 Mwanzoni mwa mwaka mpya, wakati ambapo wafalme huenda vitani, Yoabu aliliongoza jeshi. Aliangamiza nchi ya Waamoni, na akaenda Raba na kuuzingira, lakini Daudi alibaki Yerusalemu. Yoabu akashambulia Raba na kuuacha ukiwa magofu.
2 Daudi akachukua taji kutoka kwa kichwa cha mfalme wao, lililokuwa na uzito wa talanta moja ya dhahabu, nayo ilizungushiwa vito vya thamani. Ikawekwa juu ya kichwa cha Daudi. Alichukua nyara nyingi kutoka mjini huo.
3 Akawatoa watu waliokuwa humo, akawaweka wafanye kazi kwa misumeno, sululu za chuma na mashoka. Daudi akafanya hivi kwa miji yote ya Waamoni. Kisha Daudi na jeshi lake lote wakarudi Yerusalemu.
Vita Na Wafilisti
(2 Samweli 21:15-22)
4 Baada ya muda, kulitokea vita dhidi ya Wafilisti, huko Gezeri. Wakati huo Sibekai, Mhushathi, akamuua Sipai, aliyekuwa mmoja wa wazao wa Warefai, nao Wafilisti wakashindwa.
5 Katika vita vingine na Wafilisti, Elhanani mwana wa Yairi alimuua Lahmi nduguye Goliathi, Mgiti, ambaye mkuki wake ulikuwa na mpini kama mti wa mfumaji.
6 Katika vita vingine tena, vilivyopiganwa huko Gathi, kulikuwako na mtu mmoja mkubwa mwenye vidole sita katika kila mkono na vidole sita katika kila mguu: jumla vidole ishirini na vinne. Yeye alikuwa pia mzao wa Mrefai.
7 Alipowadhihaki Israeli, Yonathani, mwana wa Shimea, nduguye Daudi, akamuua.
8 Hawa walikuwa ndio wazao wa Warefai huko Gathi, nao walianguka kwa mikono ya Daudi na watu wake.