22
Ndipo Daudi akasema, “Nyumba ya Bwana Mungu itakuwa mahali hapa, pia pamoja na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya Israeli.”
Maandalizi Kwa Ajili Ya Hekalu
Kwa hiyo Daudi akatoa amri wakusanyike wageni wote waliokuwa wanaishi Israeli, na kutoka miongoni mwao akaweka waashi ili kuchonga mawe kwa ajili ya kujenga nyumba ya Mungu. Daudi akatoa chuma tele ili kutengenezea misumari kwa ajili ya mafungo ya malango ya nyumba na shaba tele isiyopimika. Pia akatoa magogo ya mierezi yasiyohesabika, kwa kuwa Wasidoni na Watiro walikuwa wamemletea Daudi idadi kubwa ya mierezi.
Daudi akasema, “Mwanangu Solomoni bado ni mdogo wa umri na hana uzoefu. Nyumba itakayojengwa kwa ajili ya Bwana inatakiwa iwe yenye uzuri mwingi na sifa na fahari mbele ya mataifa yote. Kwa hiyo nitaifanyia matayarisho.” Daudi akafanya matayarisho makubwa kabla ya kifo chake.
Kisha akamwita Solomoni mwanawe akamwagiza kujenga nyumba kwa ajili ya Bwana, Mungu wa Israeli. Daudi akamwambia Solomoni: “Mwanangu, nilikuwa na jambo hili ndani ya moyo wangu kujenga nyumba kwa ajili ya Jina la Bwana Mungu wangu. Lakini neno hili la Bwana likanijia, kusema: ‘Wewe umemwaga damu nyingi na kupigana vita vingi. Wewe hutajenga nyumba kwa ajili ya Jina langu, kwa sababu umemwaga damu nyingi juu ya nchi machoni pangu. Lakini utakuwa na mwana ambaye atakuwa mtu wa amani na utulivu nami nitampa utulivu mbele ya adui zake wote pande zote. Jina lake ataitwa Solomoni, nami nitawapa Israeli amani na utulivu wakati wa utawala wake. 10 Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya Jina langu. Yeye atakuwa mwanangu, nami nitakuwa baba yake. Nami nitakifanya imara kiti chake cha enzi cha utawala wake katika Israeli milele.’
11 “Sasa, mwanangu, Bwana awe pamoja nawe, nawe uwe na mafanikio upate kuijenga nyumba ya Bwana Mungu wako, kama alivyosema utafanya. 12 Bwana na akupe hekima na ufahamu wakati atakuweka juu ya Israeli, ili uweze kuishika sheria ya Bwana Mungu wako. 13 Ndipo utakapofanikiwa, ikiwa utakuwa na bidii kutii amri na sheria Bwana alizompa Mose kwa ajili ya Israeli. Uwe hodari na ushujaa. Usiogope wala usikate tamaa.
14 “Nimejitaabisha sana ili kupata mahitaji kwa ajili ya Hekalu la Bwana: talanta 100,000* za dhahabu, talanta 1,000,000 za fedha na kiasi kisichopimika cha shaba na chuma, pia mbao na mawe. Nawe waweza kuviongeza. 15 Unao wafanyakazi wengi: Wachonga mawe, waashi na maseremala, pamoja na watu walio na ustadi katika kila kazi 16 wa kufua dhahabu, fedha, shaba na chuma, mafundi wasiohesabika. Sasa basi anza kazi hii, naye Bwana awe pamoja nawe.”
17 Kisha Daudi akawaamuru viongozi wote wa Israeli wamsaidie Solomoni mwanawe. 18 Akawaambia, “Je, Bwana Mungu wenu si yuko pamoja na ninyi? Pia si amewapa raha pande zote? Kwa maana amewatia wenyeji wa nchi mkononi mwangu, nayo nchi iko chini ya Bwana na watu wake. 19 Sasa itoeni mioyo yenu na nafsi zenu katika kumtafuta Bwana Mungu wenu. Anzeni kujenga Maskani ya Bwana Mungu, ili mweze kulileta Sanduku la Agano la Bwana na vyombo vitakatifu vya Mungu katika Hekalu litakalojengwa kwa ajili ya Jina la Bwana.”
* 22:14 Talanta 100,000 za dhahabu ni sawa na tani 3,750. 22:14 Talanta 1,000,000 za fedha ni sawa na tani 37,500.