11
Utabiri Wa Shamaya
(1 Wafalme 12:21-24)
Ikawa Rehoboamu alipofika Yerusalemu, akakusanya nyumba ya Yuda na ya Benyamini, wanaume wapiganaji 180,000, kufanya vita dhidi ya nyumba ya Israeli na kuurudisha tena ufalme kwa Rehoboamu mwana wa Solomoni.
Lakini neno hili la Bwana likamjia Shemaya mtu wa Mungu: “Mwambie Rehoboamu mwana wa Solomoni mfalme wa Yuda, na Israeli wote walioko Yuda na Benyamini, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Msipande kupigana dhidi ya ndugu zenu. Nendeni nyumbani, kila mmoja wenu, kwa kuwa hili nimelitenda mimi.’ ” Kwa hiyo wakalitii neno la Bwana na wakaacha kwenda kupigana dhidi ya Yeroboamu.
Yeroboamu Ajengea Yuda Ngome
Rehoboamu akaishi Yerusalemu akajenga miji yenye ngome katika Yuda: Akajenga Bethlehemu, Etamu, Tekoa, Beth-Suri, Soko, Adulamu, Gathi, Maresha, Zifu, Adoraimu, Lakishi, Azeka, 10 Sora, Aiyaloni na Hebroni. Hii ndiyo iliyokuwa miji iliyojengewa ngome katika Yuda na Benyamini. 11 Akaimarisha ulinzi wake na kuweka majemadari ndani yake, pamoja na ghala za mahitaji ya vyakula, mafuta ya zeituni na divai. 12 Akaweka ngao na mikuki katika miji na kuifanya iwe imara sana. Kwa hiyo Yuda na Benyamini zikawa zake.
13 Makuhani na Walawi kutoka sehemu zote za Israeli wakawa upande wake. 14 Pia Walawi wakaacha maeneo yao ya malisho na mali zao, wakaja Yuda na Yerusalemu kwa sababu Yeroboamu na wanawe walikuwa wamewakataa wasiwe makuhani wa Bwana. 15 Naye akawa amechagua makuhani wake mwenyewe kwa ajili ya mahali pa juu pa kuabudia sanamu za mbuzi na za ndama ambazo alikuwa ametengeneza. 16 Wale waliotoka katika kila kabila la Israeli ambao walielekeza mioyo yao kumtafuta Bwana, Mungu wa Israeli, wakawafuata Walawi huko Yerusalemu kumtolea Bwana dhabihu, Mungu wa baba zao. 17 Wakaimarisha ufalme wa Yuda na kumuunga mkono Rehoboamu mwana wa Solomoni miaka mitatu, wakienenda katika njia za Daudi na Solomoni katika wakati huu.
Jamaa Ya Rehoboamu
18 Rehoboamu alimwoa Mahalati ambaye alikuwa binti Yeremothi mwana wa Daudi, mamaye alikuwa Abihaili binti Eliabu mwana wa Yese. 19 Mahalati alimzalia Rehoboamu wana: Yeushi, Shemaria na Zahamu. 20 Kisha akamwoa Maaka binti Absalomu, ambaye alimzalia: Abiya, Atai, Ziza na Shelomithi. 21 Rehoboamu akampenda Maaka binti Absalomu zaidi kuliko wakeze wengine na masuria wake. Kwa jumla alikuwa na wake kumi na wanane na masuria sitini, wana ishirini na wanane na binti sitini.
22 Rehoboamu akamweka Abiya mwana wa Maaka, kuwa mkuu wa wana wa mfalme miongoni mwa ndugu zake ili amfanye mfalme. 23 Akatenda kwa busara, akiwasambaza baadhi ya wanawe katika wilaya zote za Yuda na Benyamini, pamoja na miji yote yenye ngome. Akawapa mahitaji tele na kuwaoza wake wengi.