15
Asa Afanya Matengenezo
Roho wa Bwana akamjia Azaria mwana wa Odedi. Akatoka ili kumlaki Asa na kumwambia, “Nisikilizeni, Asa na Yuda wote na Benyamini. Bwana yu pamoja nanyi mkiwa pamoja naye. Kama mkimtafuta, ataonekana kwenu, lakini kama mkimwacha yeye, naye atawaacha ninyi. Kwa muda mrefu Israeli walikuwa hawana Mungu wa kweli, walikuwa hawana kuhani wa kuwafundisha na wala hawakuwa na sheria. Lakini katika taabu yao walimrudia Bwana, Mungu wa Israeli na kumtafuta, naye akaonekana kwao. Katika siku hizo hapakuwa na amani kwa yeyote aliyesafiri, kutoka wala kuingia, kwa kuwa wakazi wote wa nchi walikuwa katika machafuko makubwa. Taifa moja lilipigana na taifa lingine na mji mmoja ukapigana na mji mwingine, kwa sababu Mungu alikuwa anawahangaisha kwa taabu za kila aina. Lakini kwa habari yenu ninyi, kuweni hodari wala msikate tamaa, kwa kuwa mtapata thawabu kwa kazi yenu.”
Asa aliposikia maneno haya na unabii wa Azaria mwana wa Odedi nabii, akajipa moyo. Akaziondoa sanamu zote zilizokuwa machukizo katika nchi yote ya Yuda na Benyamini na kutoka miji aliyoiteka ya vilima vya Efraimu. Akakarabati madhabahu ya Bwana iliyokuwa mbele ya ukumbi wa Hekalu la Bwana.
Kisha akakutanisha Yuda wote, Benyamini na watu kutoka Efraimu, watu wa Manase na Simeoni waliokuwa wanaishi miongoni mwao, kwa maana idadi kubwa walikuwa wamemjia kutoka Israeli walipoona kwamba Bwana Mungu wake alikuwa pamoja naye.
10 Basi wakakusanyika huko Yerusalemu mwezi wa tatu katika mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Asa. 11 Wakati huo wakamtolea Bwana dhabihu za ngʼombe 700, kondoo na mbuzi 7,000 kutoka zile nyara walizoteka. 12 Wakafanya agano kumtafuta Bwana, Mungu wa baba zao kwa moyo wao wote na kwa roho yao yote. 13 Wale wote ambao hawangemtafuta Bwana, Mungu wa Israeli wangelazimika kuuawa, akiwa mdogo au mkubwa, mwanaume au mwanamke. 14 Wakamwapia Bwana kwa sauti kuu, kwa kupiga kelele, tarumbeta na kwa mabaragumu. 15 Yuda wote wakafurahia kile kiapo kwa sababu walikuwa wameapa kwa moyo wao wote. Wakamtafuta Mungu kwa bidii, naye akaonekana kwao. Kwa hiyo Bwana akawastarehesha pande zote.
16 Mfalme Asa akamwondolea Maaka mama yake wadhifa wake kama mama malkia kwa sababu alikuwa ametengeneza nguzo ya Ashera ya kuchukiza. Asa akaikata hiyo nguzo, akaivunjavunja na kuiteketeza kwa moto katika Bonde la Kidroni. 17 Ijapokuwa hakuondoa mahali pa juu pa kuabudia miungu katika Israeli, moyo wa Asa ulikuwa umejiweka kwa Bwana kikamilifu maisha yake yote. 18 Akaleta ndani ya Hekalu la Mungu fedha na dhahabu na vile vyombo ambavyo yeye na baba yake walikuwa wameviweka wakfu.
19 Hapakuwepo vita tena mpaka mwaka wa thelathini na tano wa utawala wake Asa.