30
Hezekia Aadhimisha Pasaka
Hezekia akatuma ujumbe kuwaita Israeli wote na Yuda, pia akaandika barua kwa Efraimu na Manase, kuwakaribisha ili waje hekaluni mwa Bwana huko Yerusalemu kuadhimisha Pasaka kwa Bwana, Mungu wa Israeli. Mfalme na maafisa wake pamoja na kusanyiko lote katika Yerusalemu waliamua kuadhimisha Pasaka katika mwezi wa pili. Kwa sababu makuhani hawakuwa wamejitakasa idadi ya kutosha na watu wakawa hawajakusanyika huko Yerusalemu, hawakuwa wameweza kuadhimisha Pasaka kwa wakati wake wa kawaida. Mpango huu ukaonekana wafaa kwa mfalme na kusanyiko lote. Wakaamua kupeleka tangazo Israeli kote, kuanzia Beer-Sheba hadi Dani, wakiwaita watu waje Yerusalemu kuadhimisha Pasaka ya Bwana, Mungu wa Israeli. Ilikuwa haijaadhimishwa na idadi kubwa ya watu kama hiyo kufuatana na yale yaliyokuwa yameandikwa.
Kwa amri ya mfalme, matarishi wakapita katika Israeli na Yuda kote wakiwa na barua kutoka kwa mfalme na kutoka kwa maafisa wake zikisema:
“Watu wa Israeli, mrudieni Bwana, Mungu wa Abrahamu, Isaki na Israeli, ili naye awarudie ninyi mliosalia, mlionusurika kutoka mikononi mwa wafalme wa Ashuru. Msiwe kama baba zenu na ndugu zenu, ambao hawakuwa waaminifu kwa Bwana, Mungu wa baba zao, hivyo akawafanya kitu cha kushangaza kama mnavyoona. Msiwe na shingo ngumu, kama baba zenu walivyokuwa, bali nyenyekeeni kwa Bwana. Njooni mahali patakatifu, alipopatakasa milele. Mtumikieni Bwana Mungu wenu, ili hasira yake kali igeuziwe mbali nanyi. Kama mkimrudia Bwana ndipo wale ndugu zenu waliotekwa pamoja na watoto wenu watakapoonewa huruma na wale waliowateka na kuwaachia warudi katika nchi hii, kwa kuwa Bwana Mungu wenu ni mwenye neema na huruma, hatageuzia uso wake mbali nanyi kama ninyi mkimrudia yeye.”
10 Matarishi wakaenda mji hadi mji katika Efraimu na Manase, wakafika mpaka Zabuloni, lakini watu wakawadharau na kuwadhihaki. 11 Lakini, baadhi ya watu wa Asheri, Manase na Zabuloni, wakajinyenyekeza wakaja Yerusalemu. 12 Pia katika Yuda mkono wa Mungu ulikuwa juu ya watu kuwapa umoja katika kutenda yale ambayo mfalme na maafisa wake waliwaamuru, kulingana na neno la Bwana.
13 Basi umati mkubwa wa watu ukakusanyika huko Yerusalemu kuadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu katika mwezi wa pili. 14 Wakajitia kazini kuyaondoa yale madhabahu yaliyokuwa huko Yerusalemu, wakayaondoa pia yale madhabahu ya kufukizia uvumba kwa miungu na kuyatupa Bonde la Kidroni.
15 Kisha wakamchinja mwana-kondoo wa Pasaka katika siku ya kumi na nne ya mwezi wa pili. Makuhani na Walawi waliona aibu, wakajitakasa na kuleta sadaka za kuteketezwa katika Hekalu la Bwana. 16 Kisha wakachukua nafasi zao za kawaida kama ilivyoelezwa katika Sheria ya Mose mtu wa Mungu. Makuhani wakanyunyiza ile damu waliyokabidhiwa na Walawi. 17 Kwa kuwa wengi waliokuwa katika lile kusanyiko walikuwa hawajajitakasa, iliwapasa Walawi wachinje wana-kondoo wengine wa Pasaka kwa ajili ya wale watu ambao hawakuwa safi, kwa kufuata taratibu za ibada ili kuwatakasa kwa Bwana. 18 Ingawa watu wengi miongoni mwa wale waliotoka Efraimu, Manase, Isakari na Zabuloni walikuwa hawajajitakasa, hata hivyo walikula Pasaka kinyume na ilivyoandikwa. Lakini Hezekia akawaombea, akisema, “Bwana, ambaye ni mwema na amsamehe kila mmoja 19 ambaye anauelekeza moyo wake kumtafuta Mungu, Bwana, Mungu wa baba zake, hata kama yeye si safi kulingana na sheria za mahali patakatifu.” 20 Naye Bwana akamsikia Hezekia akawaponya watu.
21 Waisraeli waliokuwa Yerusalemu wakaadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu kwa muda wa siku saba, nao Walawi na makuhani walikuwa wakiimba kila siku, wakiwa na ala za uimbaji za kumsifu Bwana.
22 Hezekia akazungumza akiwatia moyo Walawi wote, ambao walionyesha ustadi katika kumtumikia Bwana. Hivyo watu wakala chakula cha sikukuu kwa siku saba, wakitoa sadaka za amani na kumshukuru Bwana, Mungu wa baba zao.
23 Kisha kusanyiko lote likakubali kuendelea na sikukuu kwa siku saba zaidi, kwa hiyo kwa siku saba nyingine wakaendelea kuiadhimisha kwa furaha. 24 Hezekia, mfalme wa Yuda akatoa mafahali 1,000, kondoo na mbuzi 7,000 kwa ajili ya kusanyiko, nao maafisa wakatoa mafahali 1,000 pamoja na kondoo na mbuzi 10,000. Idadi kubwa ya makuhani wakajiweka wakfu. 25 Kusanyiko lote la Yuda, pamoja na makuhani na Walawi na lile kusanyiko lote lililotoka Israeli, pamoja na wale wageni waliotoka Israeli na wale walioishi katika Yuda wakafurahi. 26 Kulikuwa na furaha kubwa katika Yerusalemu, kwa sababu tangu siku za Mfalme Solomoni mwana wa Daudi mfalme wa Israeli halijakuwepo jambo kama hili katika Yerusalemu. 27 Ndipo makuhani na Walawi wakasimama wakawabariki watu, naye Mungu akawasikia, kwa sababu maombi yao yalifika mbinguni, makao yake matakatifu.