8
Shughuli Nyingine Za Solomoni
(1 Wafalme 9:10-28)
Miaka ishirini ilipopita, ambayo katika hiyo Solomoni alilijenga Hekalu la Bwana na jumba lake mwenyewe la kifalme, Solomoni akajenga tena vijiji vile ambavyo Hiramu alikuwa amempa, naye akawapa Waisraeli waishi humo. Kisha Solomoni akaenda Hamath-Soba na kuuteka. Pia akajenga mji wa Tadmori katika jangwa na miji yote ya kuhifadhia vitu katika Hamathi. Akajenga tena Beth-Horoni ya Juu na Beth-Horoni ya Chini, miji yenye ngome, kuta, malango na makomeo. Solomoni pia akajenga Baalathi na miji yake yote ya kuhifadhia vitu, na miji kwa ajili ya magari yake na kwa ajili ya farasi wake, chochote alichotaka kujenga katika Yerusalemu, katika Lebanoni na katika nchi yote aliyotawala.
Watu wote waliosalia kutoka kwa Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi (haya mataifa hayakuwa Waisraeli), yaani, wazao wao waliobakia katika nchi, ambao Waisraeli hawakuwa wamewaangamiza: hawa Solomoni akawalazimisha kuwa watumwa katika shokoa, kama ilivyo hadi leo. Lakini Solomoni hakuwafanya Waisraeli watumwa kwa ajili ya kazi yake, bali walikuwa wapiganaji, majemadari, maafisa wake, majemadari wa magari yake ya vita na waendesha magari ya vita. 10 Pia walikuwa maafisa wakuu wa Mfalme Solomoni, yaani, maafisa wakaguzi 250 waliosimamia watu.
11 Solomoni akampandisha mke wake binti Farao kutoka Mji wa Daudi na kumleta jumba la kifalme alilokuwa amemjengea, kwa kuwa alisema, “Mke wangu hataishi katika jumba la kifalme la Daudi mfalme wa Israeli, kwa sababu mahali ambapo Sanduku la Bwana limefika ni patakatifu.”
12 Mfalme Solomoni akamtolea Bwana dhabihu za kuteketezwa juu ya madhabahu ya Bwana ambayo alikuwa ameijenga mbele ya ukumbi, 13 kulingana na mahitaji ya kila siku kwa ajili ya sadaka zilizoamriwa na Mose kwa ajili ya Sabato, Mwezi Mwandamo na sikukuu nyingine tatu za mwaka, yaani, Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, Sikukuu ya Majuma na Sikukuu ya Vibanda. 14 Kwa kushika maagizo ya Daudi baba yake, aliweka migawanyo ya makuhani kwa ajili ya kazi zao, nao Walawi kuongoza kusifu na kusaidia makuhani kufuatana na mahitaji ya kila siku. Pia akaweka mabawabu katika migawanyo kwa ajili ya malango mbalimbali, kwa sababu hili ndilo Daudi mtu wa Mungu alilokuwa ameagiza. 15 Nao hawakuziacha amri za mfalme alizoamuru makuhani au Walawi katika jambo lolote, ikiwa ni pamoja na zile za hazina.
16 Kazi yote ya Mfalme Solomoni ilifanyika kuanzia siku msingi wa Hekalu la Bwana ulipowekwa mpaka kukamilika kwake. Kwa hiyo Hekalu la Bwana likamalizika kujengwa.
17 Ndipo Solomoni akaenda Esion-Geberi na Elathi katika pwani ya Edomu. 18 Naye Hiramu alimpelekea meli zilizoongozwa na maafisa wake mwenyewe, watu waliokuwa na ujuzi wa baharini. Hawa watu pamoja na wale wa Solomoni wakasafiri kwa bahari mpaka Ofiri, wakaleta kutoka huko talanta 450 za dhahabu, ambazo walimkabidhi Mfalme Solomoni.