17
Kahaba Mkuu Na Mnyama
1 Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na yale mabakuli saba akaja akaniambia, “Njoo, nitakuonyesha adhabu ya yule kahaba mkuu, aketiye juu ya maji mengi.
2 Yule ambaye wafalme wa dunia walizini naye na watu wakaao duniani walilewa kwa mvinyo wa uzinzi wake.”
3 Kisha yule malaika akanichukua katika Roho akanipeleka jangwani. Huko nikamwona mwanamke mmoja ameketi juu ya mnyama mwekundu aliyejaa majina ya kumkufuru Mungu mwili mzima. Mnyama huyo alikuwa na vichwa saba na pembe kumi.
4 Huyo mwanamke alikuwa amevaa mavazi ya rangi ya zambarau na nyekundu, akimetameta kwa dhahabu, vito vya thamani na lulu. Mkononi mwake alikuwa ameshika kikombe cha dhahabu kilichojaa mambo ya machukizo na uchafu wa uzinzi wake.
5 Kwenye kipaji chake cha uso palikuwa pameandikwa jina:
“Siri,
Babeli Mkuu,
Mama wa makahaba
na wa machukizo ya dunia.”
6 Nikaona kuwa huyo mwanamke alikuwa amelewa kwa damu ya watakatifu, yaani, damu ya wale watu waliouawa kwa ushuhuda wa Yesu.
Nilipomwona huyo mwanamke, nilistaajabu sana.
7 Ndipo yule malaika akaniambia, “Kwa nini unastaajabu? Nitakufafanulia siri ya huyo mwanamke na huyo mnyama aliyempanda, mwenye vichwa saba na pembe kumi.
8 Huyo mnyama ambaye ulimwona, wakati fulani alikuwepo, lakini sasa hayupo, naye atapanda kutoka lile Shimo na kwenda kwenye maangamizo yake. Watu waishio duniani ambao majina yao hayakuandikwa kwenye kitabu cha uzima tangu kuumbwa kwa ulimwengu watastaajabu kumwona huyo mnyama, kwa maana alikuwepo wakati fulani, na sasa hayupo, lakini atakuwepo.
9 “Hapa ndipo penye wito wa akili pamoja na hekima. Vile vichwa saba ni vilima saba ambavyo huyo mwanamke amevikalia.
10 Pia hivyo vichwa saba ni wafalme saba ambao miongoni mwao watano wamekwisha kuanguka, yupo mwingine hajaja bado, lakini atakapokuja, atalazimika kukaa kwa muda mfupi.
11 Yule mnyama aliyekuwepo wakati fulani na ambaye sasa hayupo, yeye ni mfalme wa nane. Ni miongoni mwa wale saba, naye anakwenda kwenye maangamizi yake.
12 “Zile pembe kumi ulizoziona ni wafalme kumi ambao bado hawajapokea ufalme, lakini watapokea mamlaka kuwa wafalme kwa saa moja pamoja na yule mnyama.
13 Hawa wana nia moja, nao watamwachia yule mnyama nguvu zao na mamlaka yao.
14 Watafanya vita na Mwana-Kondoo, lakini Mwana-Kondoo atawashinda kwa sababu yeye ni Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme. Yeye atakuwa pamoja na watu wake walioitwa ambao ni wateule wake na wafuasi wake waaminifu.”
15 Kisha yule malaika akaniambia, “Yale maji uliyoyaona yule kahaba akiwa ameketi juu yake ni jamaa, makutano, mataifa na lugha.
16 Zile pembe kumi ulizoziona, pamoja na huyo mnyama, watamchukia huyo kahaba, watamfilisi na kumwacha uchi, watamla nyama yake na kumteketeza kwa moto.
17 Kwa maana Mungu ameweka mioyoni mwao kutimiza kusudi lake kwa kukubali kumpa yule mnyama mamlaka yao ya utawala mpaka maneno ya Mungu yatakapotimia.
18 Yule mwanamke uliyemwona ni ule mji mkubwa unaotawala juu ya wafalme wa dunia.”