22
Mto Wa Maji Ya Uzima
1 Kisha yule malaika akanionyesha mto wa maji ya uzima, maangavu kama kioo yakitiririka kutoka kwenye kile kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo,
2 kupitia katikati ya barabara kuu ya huo mji. Kwenye kila upande wa huo mto kulikuwa na mti wa uzima utoao matunda ya aina kumi na mbili, ukizaa matunda yake kila mwezi. Nayo majani ya mti huo ni kwa ajili ya uponyaji wa mataifa.
3 Katika mji huo hakutakuwa tena na laana, bali kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo kitakuwamo humo na watumishi wake watamtumikia,
4 nao watamwona uso wake na Jina lake litakuwa kwenye vipaji vya nyuso zao.
5 Usiku hautakuwako tena, wala hawatahitaji mwanga wa taa au wa jua, kwa maana Bwana Mungu atakuwa nuru yao, nao watatawala milele na milele.
6 Kisha yule malaika akaniambia, “Maneno haya ni ya kuaminika na kweli. Bwana, Mungu wa roho za manabii, alimtuma malaika wake kuwaonyesha watumishi wake yale ambayo hayana budi kutukia upesi.”
Bwana Yesu Anakuja
7 “Tazama, naja upesi! Amebarikiwa yeye ayashikaye maneno ya unabii wa kitabu hiki.”
8 Mimi, Yohana, ndiye niliyesikia na kuyaona mambo haya. Nami nilipokwisha kuyasikia na kuyaona, nilianguka chini nikasujudu miguuni pa yule malaika aliyekuwa akinionyesha mambo hayo.
9 Lakini yeye akaniambia, “Usifanye hivyo! Mimi ni mtumishi pamoja nawe na ndugu zako manabii na wote wanaoyashika maneno ya kitabu hiki. Msujudie Mungu!”
10 Kisha akaniambia, “Usiyafunge maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, kwa sababu wakati umekaribia.
11 Atendaye mabaya na aendelee kutenda mabaya, aliye mchafu na aendelee kuwa mchafu, yeye atendaye haki na aendelee kutenda haki, na yeye aliye mtakatifu na aendelee kuwa mtakatifu.”
12 “Tazama, naja upesi! Thawabu yangu i mkononi mwangu, nami nitampa kila mtu sawasawa na alivyotenda.
13 Mimi ni Alfa na Omega, wa Kwanza na wa Mwisho, Mwanzo na Mwisho.
14 “Wamebarikiwa wale wafuao mavazi yao, ili wapate haki ya kuuendea huo mti wa uzima na kuuingia huo mji kupitia kwenye malango yake.
15 Huko nje wako mbwa, wachawi, wazinzi, wauaji, waabudu sanamu, na kila mtu apendaye udanganyifu na kuufanya.
16 “Mimi, Yesu, nimemtuma malaika wangu kushuhudia mambo haya kwa ajili ya makanisa. Mimi ndimi Shina na Mzao wa Daudi, ile Nyota ya Asubuhi ingʼaayo.”
17 Roho na bibi arusi wanasema, “Njoo!” Naye asikiaye na aseme, “Njoo!” Yeyote mwenye kiu na aje, na kila anayetaka na anywe maji ya uzima bure.
18 Namwonya kila mtu asikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki: Mtu yeyote akiongeza humo chochote, Mungu atamwongezea mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki.
19 Kama mtu yeyote akipunguza humo chochote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.
20 Yeye anayeshuhudia mambo haya asema, “Hakika, naja upesi!”
Amen. Njoo, Bwana Yesu.
21 Neema ya Bwana Yesu iwe na watakatifu wote. Amen.