17
Daudi Na Goliathi
Wakati huu Wafilisti wakakusanya majeshi yao kwa ajili ya vita, nao wakakusanyika huko Soko katika Yuda. Wakapiga kambi huko Efes-Damimu, kati ya Soko na Azeka. Sauli na Waisraeli wakakusanyika na kupiga kambi katika Bonde la Ela na kupanga jeshi ili kupigana vita na Wafilisti. Wafilisti wakawa katika kilima kimoja na Waisraeli katika kilima kingine, hilo bonde likiwa kati yao.
Shujaa aliyeitwa Goliathi, aliyetoka Gathi, akajitokeza kutoka kambi ya Wafilisti. Alikuwa na urefu dhiraa sita na shibiri moja.* Alikuwa na chapeo ya shaba kichwani mwake, na alivaa dirii ya shaba kifuani mwake yenye uzito wa shekeli elfu tano. Miguuni mwake alivaa mabamba ya shaba, na alikuwa na mkuki wa shaba mgongoni mwake. Mpini wa huo mkuki ulikuwa kama mti wa mfumaji, na ncha ya chuma yake ilikuwa na uzito wa shekeli mia sita. Mbeba ngao wake alitangulia mbele yake.
Goliathi alisimama na kuwapigia kelele majeshi ya Israeli, akisema, “Kwa nini mmetoka kupanga vita? Je, mimi si Mfilisti, na ninyi ni watumishi wa Sauli? Chagueni mtu na anishukie mimi. Kama anaweza kupigana nami na kuniua, tutakuwa chini yenu; lakini kama nikimshinda na kumuua, ninyi mtakuwa chini yetu na mtatutumikia.” 10 Kisha yule Mfilisti akasema, “Siku hii ya leo nayatukana majeshi ya Israeli! Nipeni mtu tupigane.” 11 Kwa kusikia maneno ya Wafilisti, Sauli na Waisraeli wote wakafadhaika na kuogopa.
12 Basi Daudi alikuwa mwana wa Mwefrathi jina lake Yese aliyekuwa ametoka Bethlehemu ya Yuda. Yese alikuwa na wana wanane, naye wakati wa Sauli alikuwa mzee tena wa umri mkubwa. 13 Wana wakubwa watatu wa Yese walikuwa wamefuatana na Sauli vitani: Mzaliwa wa kwanza alikuwa Eliabu, wa pili Abinadabu, na wa tatu Shama. 14 Daudi ndiye alikuwa mdogo wa wote. Hao wakubwa watatu wakamfuata Sauli, 15 lakini Daudi alikuwa akienda kwa Sauli na kurudi ili kuchunga kondoo wa baba yake huko Bethlehemu.
16 Kwa siku arobaini huyo Mfilisti alikuwa akija mbele kila siku asubuhi na jioni na kujionyesha.
17 Wakati huo Yese akamwambia mwanawe Daudi, “Chukua hii efa§ ya bisi na hii mikate kumi kwa ajili ya ndugu zako uwapelekee upesi kambini mwao. 18 Chukua pamoja na hizi jibini kumi kwa jemadari wa kikosi chao. Ujue hali ya ndugu zako na uniletee taarifa za uhakika kutoka kwao. 19 Wao wako pamoja na Sauli na watu wote wa Israeli huko kwenye Bonde la Ela, wakipigana na Wafilisti.”
20 Asubuhi na mapema Daudi akaondoka, akaliacha kundi la kondoo pamoja na mchungaji, akapakia vitu vile na kuondoka, kama vile Yese alivyokuwa amemwagiza. Akafika kambini wakati jeshi lilikuwa likitoka kwenda kwenye sehemu yake ya kupigania, huku wakipiga kelele za vita. 21 Israeli na Wafilisti walikuwa wakipanga safu zao wakitazamana. 22 Daudi akaacha vile vitu vyake kwa mtunza vifaa, akakimbilia katika safu za vita na kuwasalimu ndugu zake. 23 Alipokuwa akisema nao, Goliathi, yule Mfilisti shujaa kutoka Gathi, akajitokeza mbele ya safu zake na kupiga ile kelele yake ya kawaida ya matukano, naye Daudi akayasikia. 24 Waisraeli walipomwona yule mtu, wote wakamkimbia kwa woga mkuu.
25 Basi Waisraeli walikuwa wakisema, “Je, mnaona jinsi mtu huyu anavyoendelea kujitokeza. Hujitokeza ili kutukana Israeli. Mfalme atatoa utajiri mwingi kwa yule mtu atakayemuua. Pia atamwoza binti yake na atasamehe jamaa ya baba yake kulipa kodi katika Israeli.”
26 Daudi akauliza watu waliokuwa wamesimama karibu naye, “Je, atafanyiwa nini mtu atakayemuua huyu Mfilisti na kuondoa aibu hii katika Israeli? Ni nani huyu Mfilisti asiyetahiriwa hata atukane majeshi ya Mungu aliye hai?”
27 Wakarudia yale yaliyokuwa yamesemwa na kumwambia kuwa, “Hili ndilo atakalotendewa mtu yule atakayemuua.”
28 Eliabu nduguye mkubwa Daudi alipomsikia akizungumza na watu hasira ikawaka juu yake akamuuliza, “Kwa nini umeteremka kuja hapa? Nao wale kondoo wachache kule nyikani umewaacha na nani? Ninajua jinsi ulivyo na kiburi na jinsi moyo wako ulivyo mwovu; umekuja hapa kutazama vita tu.”
29 Daudi akasema, “Sasa nimefanya nini? Je, siwezi hata kuongea.” 30 Daudi akamgeukia mtu mwingine na kumuuliza jambo lilo hilo, nao watu wakamjibu vilevile kama mwanzo. 31 Lile Daudi alilosema likasikiwa na kuelezwa kwa Sauli, naye Sauli akatuma aitwe.
32 Daudi akamwambia Sauli, “Mtu yeyote asife moyo kwa habari ya huyu Mfilisti; mtumishi wako atakwenda kupigana naye.”
33 Sauli akamjibu Daudi, “Wewe hutaweza kwenda kupigana dhidi ya huyu Mfilisti; wewe ni kijana tu, naye amekuwa mtu wa vita tangu ujana wake.”
34 Lakini Daudi akamwambia Sauli, “Mtumishi wako amekuwa akichunga kondoo wa baba yake. Wakati simba au dubu alikuja na kuchukua kondoo kutoka kundi, 35 nilifuatia, nikampiga na nikampokonya kondoo kwenye kinywa chake. Aliponigeukia, nilimkamata nywele zake, nikampiga na kumuua. 36 Mtumishi wako ameshaua simba na dubu pia; huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wa hao, kwa sababu ameyatukana majeshi ya Mungu aliye hai. 37  Bwana ambaye aliniokoa toka katika makucha ya simba na makucha ya dubu ataniokoa kutoka mikono ya huyu Mfilisti.”
Sauli akamwambia Daudi, “Nenda, naye Bwana na awe pamoja nawe.”
38 Ndipo Sauli akamvika Daudi silaha zake mwenyewe za vita. Akamvika dirii na chapeo ya shaba kichwani mwake. 39 Daudi akajifunga upanga juu ya hayo mavazi na kujaribu kutembea kwa sababu alikuwa hana uzoefu navyo.
Daudi akamwambia Sauli, “Siwezi kwenda nikiwa nimevaa hivi, kwa sababu sina uzoefu navyo.” Hivyo akavivua. 40 Kisha akachukua fimbo yake mkononi, akachagua mawe laini matano kutoka kwenye kijito, akayaweka kwenye kifuko ndani ya mfuko wake wa kichungaji, akiwa na kombeo yake mkononi mwake, akamkaribia yule Mfilisti.
41 Wakati ule ule, yule Mfilisti, akiwa na mbeba ngao wake mbele yake, akaendelea kujongea karibu na Daudi. 42 Mfilisti akamwangalia Daudi kote na kumwona kuwa ni kijana tu, mwekundu na mzuri wa kupendeza, naye akamdharau. 43 Akamwambia Daudi, “Je, mimi ni mbwa, hata unanijia na fimbo?” Yule Mfilisti akamlaani Daudi kwa miungu yake. 44 Tena Mfilisti akamwambia, “Njoo hapa, nami nitawapa ndege wa angani na wanyama wa mwituni nyama yako.”
45 Daudi akamwambia yule Mfilisti. “Wewe unanijia na upanga, mkuki na fumo, lakini mimi ninakujia kwa jina la Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa majeshi ya Israeli, ambaye wewe umemtukana. 46 Siku hii leo Bwana atakutia mkononi mwangu, nami nitakupiga na kukukata kichwa chako. Leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya jeshi la Wafilisti, nayo dunia yote itajua kuwa yuko Mungu katika Israeli. 47 Wale wote waliokusanyika hapa watajua kuwa Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; kwa kuwa vita ni vya Bwana, naye atawatia wote mikononi mwetu.”
48 Yule Mfilisti aliposogea karibu ili kumshambulia, Daudi akaenda mbio kuelekea safu ya vita kukutana naye. 49 Daudi akatia mkono wake mfukoni na kuchukua jiwe, akalirusha kwa kombeo, nalo likampiga yule Mfilisti kwenye paji la uso. Lile jiwe likaingia kipajini mwa uso, akaanguka chini kifudifudi.
50 Basi Daudi akamshinda huyo Mfilisti kwa kombeo na jiwe; bila kuwa na upanga mikononi mwake akampiga huyo Mfilisti na kumuua.
51 Daudi akakimbia na kusimama juu yake. Akaushika upanga wa huyo Mfilisti na kuuvuta toka kwenye ala yake. Baada ya kumuua, akakata kichwa chake kwa ule upanga.
Wafilisti walipoona kuwa shujaa wao amekufa, wakageuka na kukimbia. 52 Ndipo watu wa Israeli na Yuda wakainuka kwenda mbele wakipiga kelele na kufuatia Wafilisti mpaka kwenye ingilio la Gathi kwenye malango ya Ekroni. Maiti zao zilitawanyika kando ya barabara ya Shaaraimu hadi Gathi na Ekroni. 53 Waisraeli waliporudi kutoka kuwafukuza Wafilisti, waliteka nyara kutoka kambi yao. 54 Daudi akachukua kichwa cha yule Mfilisti na kukileta Yerusalemu, naye akaweka silaha za huyo Mfilisti katika hema lake mwenyewe.
55 Sauli alipomwona Daudi anakwenda kukabiliana na huyo Mfilisti, alimwambia Abneri, jemadari wa jeshi, “Abneri, yule kijana ni mwana wa nani?”
Abneri akajibu, “Hakika kama uishivyo, ee mfalme, mimi sifahamu.”
56 Mfalme akasema, “Uliza huyu kijana ni mwana wa nani.”
57 Mara Daudi aliporudi kutoka kumuua huyo Mfilisti, Abneri akamchukua na kumleta mbele ya Sauli. Daudi alikuwa bado anakishikilia kichwa cha yule Mfilisti.
58 Sauli akamuuliza, “Kijana, wewe ni mwana wa nani?”
Daudi akasema, “Mimi ni mwana wa mtumishi wako Yese wa Bethlehemu.”
* 17:4 Dhiraa sita na shibiri moja ni sawa na mita 3, au futi 9 na inchi 8. 17:5 Shekeli 15,000 ni sawa na kilo 50. 17:7 Shekeli 600 ni sawa na kilo 7. § 17:17 Efa moja ni sawa na kilo 22.