16
Daudi Na Siba
1 Daudi alipokuwa amekwenda umbali mfupi kupita kilele cha mlima, akamkuta huko Siba, msimamizi wa shughuli za Mefiboshethi, akingojea kumlaki Daudi. Alikuwa na punda wawili wakiwa wametandikwa na kupakiwa mikate mia mbili, maandazi mia ya zabibu kavu, maandazi mia ya tini na kiriba cha divai.
2 Mfalme Daudi akamuuliza Siba, “Kwa nini umeleta vitu hivi?”
Siba akamjibu, “Punda ni kwa ajili ya watu wa nyumba ya mfalme kupanda, mikate na matunda ni kwa ajili ya watu kula, nayo divai ni kwa kuwaburudisha watakaochoka jangwani.”
3 Kisha mfalme akauliza, “Yuko wapi mwana wa bwana wako?”
Siba akamwambia, “Anakawia Yerusalemu, kwa sababu anafikiri, ‘Leo nyumba ya Israeli itanirudishia utawala wa baba yangu.’ ”
4 Ndipo mfalme akamwambia Siba, “Yote yaliyokuwa mali ya Mefiboshethi sasa ni mali yako.”
Siba akasema, “Nasujudu kwa unyenyekevu. Naomba nipate kibali mbele yako, bwana wangu mfalme.”
Shimei Amlaani Daudi
5 Mfalme Daudi alipokuwa anakaribia Bahurimu, mtu mmoja kutoka ukoo huo huo kama jamaa ya Sauli, akatoka humo, ambaye jina lake ni Shimei mwana wa Gera; akawa analaani alipokuwa akitoka.
6 Akamtupia Daudi na maafisa wote wa mfalme mawe, ingawa vikosi vyote na walinzi maalum walikuwa kulia na kushoto mwa Daudi.
7 Shimei alivyokuwa akilaani, akasema, “Toka hapa, toka hapa, wewe mtu wa damu, wewe mtu mbaya kabisa!
8 Bwana amekulipiza kwa ajili ya damu yote uliyomwaga ya watu wa nyumba ya Sauli, ambaye nafasi yake umeimiliki wewe. Bwana amekabidhi ufalme mkononi mwa mwanao Absalomu. Maangamizi yamekupata kwa sababu wewe ni mtu wa damu!”
9 Ndipo Abishai mwana wa Seruya akamwambia mfalme, “Kwa nini huyu mbwa mfu amlaani bwana wangu mfalme? Niruhusu nivuke nikatilie mbali kichwa chake.”
10 Lakini mfalme akamwambia, “Mna nini nami, enyi wana wa Seruya? Ikiwa analaani kwa sababu Bwana amemwambia, ‘Mlaani Daudi,’ nani awezaye kuuliza, ‘Kwa nini unafanya hivi?’ ”
11 Ndipo Daudi akamwambia Abishai na maafisa wake wote, “Mwanangu, yeye ambaye ametoka viunoni mwangu mwenyewe, anajaribu kuuondoa uhai wangu. Je, si zaidi sana kwa huyu Mbenyamini! Mwacheni, acha alaani, kwa maana Bwana amemwambia afanye hivyo.
12 Inawezekana kwamba Bwana ataona dhiki yangu na kunilipa mema kwa ajili ya laana ninayopokea leo.”
13 Kwa hiyo Daudi na watu wake wakaendelea na safari yao barabarani, huku Shimei akiwa anatembea pembezoni mwa kilima sambamba na Daudi, huku akimlaani na kumtupia Daudi mawe na kumrushia mavumbi.
14 Mfalme na watu wote aliokuwa pamoja nao wakafika kwenye kituo chao wakiwa wamechoka. Mfalme akajiburudisha hapo.
Shauri La Hushai Na Ahithofeli
15 Wakati huo, Absalomu pamoja na watu wote wa Israeli wakafika Yerusalemu, naye Ahithofeli alikuwa pamoja naye.
16 Ndipo Hushai, Mwariki, rafiki wa Daudi, akamwendea Absalomu na kumwambia, “Mfalme aishi maisha marefu! Mfalme aishi maisha marefu!”
17 Absalomu akamuuliza Hushai, “Je, huu ndio upendo unaomwonyesha rafiki yako? Kwa nini hukufuatana na rafiki yako?”
18 Hushai akamwambia Absalomu, “La hasha, yeye aliyechaguliwa na Bwana, aliyechaguliwa na watu hawa, atakayechaguliwa tena na watu wote wa Israeli, huyu ndiye nitakayekuwa wake, nami nitabakia pamoja naye.
19 Zaidi ya hayo, nimtumikie nani? Je, nisimtumikie mwana? Kama vile nilivyomtumikia baba yako, ndivyo nitakavyokutumikia wewe.”
20 Absalomu akamwambia Ahithofeli, “Tupe shauri lako. Tufanye nini?”
21 Ahithofeli akamjibu, “Kutana kimwili na masuria wa baba yako aliowaacha kutunza jumba la kifalme. Ndipo Israeli yote itakaposikia kwamba umejifanya chukizo kwa baba yako, nayo mikono ya kila mmoja aliye pamoja nawe itatiwa nguvu.”
22 Kwa hiyo wakasimika hema kwa ajili ya Absalomu juu ya paa, naye akakutana kimwili na masuria wa baba yake mbele ya Israeli wote.
23 Ilikuwa katika siku hizo shauri lililotolewa na Ahithofeli lilikuwa kama lile ambalo limeulizwa kwa Mungu. Ndivyo Daudi na Absalomu walivyoyaheshimu mashauri yote ya Ahithofeli.