22
Wimbo Wa Daudi Wa Sifa
(Zaburi 18)
1 Daudi alimwimbia Bwana maneno ya wimbo huu wakati Bwana alipomwokoa mikononi mwa adui zake wote, na pia mkononi mwa Sauli.
2 Akasema:
“Bwana ni mwamba wangu,
ngome yangu na mwokozi wangu,
3 Mungu wangu ni mwamba wangu,
ambaye kwake ninakimbilia,
ngao yangu na pembe ya wokovu wangu.
Yeye ni ngome yangu, kimbilio langu
na mwokozi wangu,
huniokoa kutoka kwa watu wenye jeuri.
4 Ninamwita Bwana, anayestahili kusifiwa,
nami ninaokolewa kutoka kwa adui zangu.
5 “Mawimbi ya mauti yalinizunguka,
mafuriko ya maangamizi yalinilemea.
6 Kamba za kuzimu zilinizunguka,
mitego ya mauti ilinikabili.
7 Katika shida yangu nalimwita Bwana,
nilimlilia Mungu wangu.
Kutoka Hekaluni mwake alisikia sauti yangu,
kilio changu kikafika masikioni mwake.
8 “Dunia ilitetemeka na kutikisika,
misingi ya mbingu ikatikisika,
vilitetemeka kwa sababu
alikuwa amekasirika.
9 Moshi ukapanda kutoka puani mwake,
moto uteketezao ukatoka kinywani mwake,
makaa ya moto yawakayo
yakatoka ndani mwake.
10 Akazipasua mbingu akashuka chini,
mawingu meusi yalikuwa chini ya miguu yake.
11 Alipanda juu ya kerubi akaruka,
akapaa juu kwa mbawa za upepo.
12 Alifanya giza hema lake la kujifunika:
mawingu meusi ya mvua ya angani.
13 Kutokana na mwanga wa uwepo wake
mawingu yalisogea,
ikanyesha mvua ya mawe
na umeme wa radi.
14 Bwana alinguruma kutoka mbinguni,
sauti ya Aliye Juu Sana ilisikika.
15 Aliipiga mishale na kutawanya adui,
umeme wa radi na kuwafukuza.
16 Mabonde ya bahari yalifunuliwa,
na misingi ya dunia ikawa wazi
kwa kukaripia kwake Bwana,
kwa uvumi wa pumzi kutoka puani mwake.
17 “Alinyoosha mkono kutoka juu na kunishika;
alinitoa kutoka kilindi cha maji makuu.
18 Aliniokoa kutoka adui wangu mwenye nguvu nyingi,
kutoka adui zangu waliokuwa na nguvu nyingi kuliko mimi.
19 Walinikabili siku ya msiba wangu,
lakini Bwana alikuwa msaada wangu.
20 Alinileta nje mahali penye nafasi tele,
akaniokoa kwa kuwa alipendezwa nami.
21 “Bwana alinitendea sawasawa na uadilifu wangu;
sawasawa na usafi wa mikono yangu amenilipa.
22 Kwa maana nimezishika njia za Bwana;
sijatenda ubaya nikamwacha Mungu wangu.
23 Sheria zake zote zi mbele yangu,
wala sijayaacha maagizo yake.
24 Nimekuwa sina hatia mbele zake,
nami nimejilinda nisitende dhambi.
25 Bwana amenilipa sawasawa na uadilifu wangu,
sawasawa na usafi wangu machoni pake.
26 “Kwa yeye aliye mwaminifu unajionyesha kuwa mwaminifu,
kwa asiye na hatia unajionyesha kutokuwa na hatia,
27 kwa aliye mtakatifu unajionyesha kuwa mtakatifu,
lakini kwa aliyepotoka unajionyesha kuwa mkaidi.
28 Wewe huwaokoa wanyenyekevu,
lakini macho yako ni juu ya wenye kiburi
ili uwashushe.
29 Wewe ni taa yangu, Ee Bwana.
Bwana hulifanya giza langu
kuwa mwanga.
30 Kwa msaada wako naweza kushinda jeshi,
nikiwa pamoja na Mungu wangu
nitaweza kuruka ukuta.
31 “Kuhusu Mungu, njia yake ni kamilifu;
neno la Bwana halina dosari.
Yeye ni ngao kwa wote
wanaokimbilia kwake.
32 Kwa maana ni nani aliye Mungu
zaidi ya Bwana?
Ni nani aliye Mwamba
isipokuwa Mungu wetu?
33 Mungu ndiye anivikaye nguvu
na kufanya njia yangu kuwa kamilifu.
34 Huifanya miguu yangu kama miguu ya kulungu,
huniwezesha kusimama mahali palipo juu.
35 Huifundisha mikono yangu kupigana vita;
mikono yangu inaweza kupinda upinde wa shaba.
36 Hunipa ngao yako ya ushindi,
unajishusha chini ili kuniinua.
37 Huyapanua mapito yangu,
ili miguu yangu isiteleze.
38 “Niliwafuatia adui zangu na nikawaseta,
sikurudi nyuma mpaka walipoangamizwa.
39 Niliwaseta kabisa, nao hawakuweza kuinuka tena;
walianguka chini ya miguu yangu.
40 Ulinivika nguvu kwa ajili ya kupigana vita;
uliwafanya adui zangu wasujudu miguuni pangu.
41 Uliwafanya adui zangu wageuke na kukimbia,
nami nikawaangamiza adui zangu.
42 Walipiga yowe, lakini hapakuwepo na yeyote wa kuwaokoa;
walimlilia Bwana, lakini hakuwajibu.
43 Niliwaponda kama mavumbi ya nchi;
niliwaponda na kuwakanyaga kama tope barabarani.
44 “Umeniokoa kutokana na mashambulizi ya watu wangu;
umenihifadhi mimi kama kiongozi wa mataifa.
Watu ambao sikuwajua wananitumikia,
45 nao wageni huja wakininyenyekea,
mara wanisikiapo, hunitii.
46 Wote wanalegea,
wanatoka katika ngome zao wakitetemeka.
47 “Bwana yu hai! Sifa ni kwa Mwamba wangu!
Atukuzwe Mungu,
Mwamba, Mwokozi wangu!
48 Yeye ndiye Mungu anilipiziaye kisasi,
ayawekaye mataifa chini yangu,
49 aniwekaye huru toka kwa adui zangu.
Uliniinua juu ya adui zangu;
uliniokoa toka kwa watu wajeuri.
50 Kwa hiyo nitakusifu, Ee Bwana,
katikati ya mataifa;
nitaliimbia sifa jina lako.
51 Humpa mfalme wake ushindi mkuu;
huonyesha fadhili zake kwa mpakwa mafuta wake,
kwa Daudi na wazao wake milele.”