6
Sanduku La Mungu Laletwa Yerusalemu
(1 Nyakati 13:1-14; 15:25–16:6, 43)
1 Tena Daudi akakusanya watu 30,000 wa Israeli waliochaguliwa.
2 Yeye na watu wake wote wakatoka Baala ya Yuda kulipandisha Sanduku la Mungu kutoka huko, linaloitwa kwa Jina, naam, jina la Bwana Mwenye Nguvu Zote, ambaye anaketi katika kiti cha enzi kati ya makerubi walioko juu ya hilo Sanduku.
3 Wakaweka hilo Sanduku la Mungu juu ya gari jipya la kukokotwa na kulileta kutoka nyumba ya Abinadabu, iliyokuwa juu ya kilima. Uza na Ahio, wana wa Abinadabu, walikuwa wakiongoza hilo gari jipya la kukokotwa
4 likiwa na Sanduku la Mungu juu yake, naye Ahio alikuwa anatembea akiwa mbele yake.
5 Daudi na nyumba yote ya Israeli walikuwa wanacheza mbele za Bwana kwa nguvu zao zote, kwa nyimbo, vinubi, zeze, matari, kayamba na matoazi.
6 Walipofika kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Nakoni, Uza akanyoosha mkono na kulishika Sanduku la Mungu kwa sababu maksai walijikwaa.
7 Hasira ya Bwana ikawaka dhidi ya Uza kwa sababu ya kitendo chake cha kukosa heshima, kwa hiyo Mungu akampiga akafia papo hapo kando ya Sanduku la Mungu.
8 Ndipo Daudi akakasirika kwa sababu ghadhabu ya Bwana ilifurika dhidi ya Uza, hivyo hadi leo mahali hapo panaitwa Peres-Uza.
9 Daudi akamwogopa Bwana siku ile, akasema, “Ni jinsi gani Sanduku la Bwana litakavyoweza kunijia?”
10 Hakuwa radhi kulichukua Sanduku la Bwana kwake katika Mji wa Daudi. Badala yake akalipeleka kwenye nyumba ya Obed-Edomu, Mgiti.
11 Sanduku la Bwana likabaki katika nyumba ya Obed-Edomu, Mgiti, kwa miezi mitatu, naye Bwana akambariki pamoja na nyumba yake yote.
12 Kisha Mfalme Daudi akaambiwa, “Bwana ameibariki nyumba ya Obed-Edomu pamoja na kila alicho nacho, kwa sababu ya Sanduku la Mungu.” Basi Daudi akateremka na kulipandisha Sanduku la Mungu kutoka nyumba ya Obed-Edomu hadi Mji wa Daudi kwa shangwe.
13 Wale waliokuwa wamebeba Sanduku la Bwana walipokuwa wametembea hatua sita, Daudi alitoa dhabihu fahali na ndama aliyenoneshwa.
14 Daudi, akiwa amevaa kisibau cha kitani, alicheza mbele za Bwana kwa nguvu zake zote,
15 wakati yeye na nyumba yote ya Israeli walipopandisha Sanduku la Bwana kwa shangwe na sauti za tarumbeta.
16 Ikawa Sanduku la Bwana lilipokuwa linaingia katika Mji wa Daudi, Mikali binti Sauli akachungulia dirishani. Naye alipomwona Mfalme Daudi akirukaruka na kucheza mbele za Bwana, akamdharau moyoni mwake.
17 Wakaleta Sanduku la Bwana na kuliweka mahali pake ndani ya hema ambalo Daudi alikuwa amelisimamisha kwa ajili yake, naye Daudi akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za Bwana.
18 Baada ya kumaliza kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani, Daudi akawabariki watu katika jina la Bwana Mwenye Nguvu Zote.
19 Kisha akatoa mkate, andazi la tende na andazi la zabibu kavu kwa kila mtu katika mkutano wote wa Waisraeli, wanaume kwa wanawake. Nao watu wote wakaenda nyumbani kwao.
20 Daudi aliporudi ili kuwabariki watu wa nyumbani mwake, Mikali binti Sauli akatoka nje kumlaki, akamwambia, “Tazama jinsi mfalme wa Israeli alivyojibainisha mwenyewe leo kwa kuvua mavazi yake machoni pa vijakazi wa watumishi wake, kama vile ambavyo mtu asiye na adabu angelifanya!”
21 Daudi akamwambia Mikali, “Nilifanya hivyo mbele za Bwana ambaye alinichagua mimi badala ya baba yako au mwingine yeyote kutoka nyumba yake wakati aliponiweka niwe mtawala juu ya Israeli, watu wa Bwana. Kwa hiyo nitacheza mbele za Bwana.
22 Nitakuwa asiye na heshima zaidi kuliko sasa, nami nitajishusha machoni pangu mwenyewe. Lakini kwa hawa vijakazi uliosema habari zao nitaheshimiwa.”
23 Naye Mikali binti Sauli hakuwa na watoto mpaka siku ya kufa kwake.