10
Kifo cha Nadabu na Abihu
Nadabu na Abihu, wana wa Haruni, wakachukua vyetezo vyao, wakaweka moto ndani yake na kuongeza uvumba; kisha wakamtolea Mwenyezi Mungu moto usio halali, kinyume na agizo la Mungu. Hivyo moto ukaja kutoka kwa uwepo wa Mwenyezi Mungu na kuwateketeza, nao wakafa mbele za Mwenyezi Mungu. Kisha Musa akamwambia Haruni, “Hili ndilo alilonena Mwenyezi Mungu, aliposema:
“ ‘Miongoni mwa wale watakaonikaribia
nitajionesha kuwa mtakatifu;
machoni pa watu wote
nitaheshimiwa.’ ”
Haruni akanyamaza.
Musa akawaita Mishaeli na Elisafani, wana wa Uzieli mjomba wake Haruni, akawaambia, “Njooni hapa. Ondoeni miili ya ndugu zenu mbele ya mahali patakatifu, mkaipeleke nje ya kambi.” Hivyo wakaja na kuwaondoa, wakiwa bado wamevalia makoti yao ya ibada, wakawapeleka nje ya kambi, kama Musa alivyoamuru.
Ndipo Musa akamwambia Haruni pamoja na wanawe, Eleazari na Ithamari, “Msifunue vichwa vyenu wala msirarue mavazi yenu, la sivyo mtakufa na Mwenyezi Mungu ataikasirikia jumuiya nzima. Lakini ndugu zenu, nyumba yote ya Israeli, wanaweza kuwaombolezea wale ambao Mwenyezi Mungu amewaangamiza kwa moto. Msitoke nje ya ingilio la Hema la Kukutania, la sivyo mtakufa, kwa sababu mafuta ya Mwenyezi Mungu ya upako yako juu yenu.” Hivyo wakafanya kama vile Musa alivyosema.
Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Haruni, “Wewe na wanao msinywe mvinyo wala kinywaji kingine kilichochachuka wakati mwingiapo katika Hema la Kukutania, la sivyo mtakufa. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo. 10 Ni lazima mtenganishe kati ya kilicho kitakatifu na kilicho cha kawaida, kati ya kilicho najisi na kilicho safi, 11 na lazima mwafundishe Waisraeli amri zote ambazo Mwenyezi Mungu aliwapa kupitia Musa.”
12 Musa akamwambia Haruni pamoja na wanawe waliosalia, Eleazari na Ithamari, “Chukueni sadaka ya nafaka iliyobaki kutoka kwa sadaka zilizotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto, muile hapo kando ya madhabahu ikiwa imeandaliwa bila chachu, kwa sababu ni takatifu sana. 13 Mtaila katika mahali patakatifu kwa sababu ni fungu lenu na fungu la wana wenu la sadaka zilizotolewa kwa Mwenyezi Mungu kwa moto, kwa maana hivyo ndivyo nilivyoamriwa. 14 Lakini wewe na wanao na binti zako mwaweza kula kidari kile kilichoinuliwa na paja lile lililotolewa. Mtavila katika mahali patakatifu; mmepewa wewe na wanao kuwa fungu lenu la sadaka za amani za Waisraeli. 15 Paja lile lililotolewa na kidari kile kilichoinuliwa lazima viletwe pamoja na sehemu za mafuta ya wanyama wa sadaka za kuteketezwa kwa moto, ili kuinuliwa mbele za Mwenyezi Mungu kuwa sadaka ya kuinuliwa. Hili litakuwa fungu lako na wanao milele, kama Mwenyezi Mungu alivyoagiza.”
16 Musa alipouliza kuhusu mbuzi aliyetolewa sadaka ya dhambi na kugundua kwamba ameteketezwa, aliwakasirikia Eleazari na Ithamari, wana wa Haruni waliobaki. Akawauliza, 17 “Kwa nini hamkula sadaka ya dhambi katika eneo la mahali patakatifu? Ni takatifu sana. Mlipewa ninyi ili kuondoa hatia ya jumuiya kwa ajili ya kuwafanyia upatanisho mbele za Mwenyezi Mungu. 18 Kwa kuwa damu yake haikuletwa ndani ya Mahali Patakatifu, mngemla mbuzi huyo katika sehemu ya mahali patakatifu kama nilivyoagiza.”
19 Haruni akamjibu Musa, “Leo wanangu wametoa sadaka zao za dhambi na sadaka zao za kuteketezwa mbele za Mwenyezi Mungu, lakini mambo kama haya yamenitokea mimi. Je, Mwenyezi Mungu angependezwa kama ningekuwa nimekula sadaka ya dhambi leo?” 20 Musa aliposikia haya, akaridhika.