21
1 Yahwe akamsikiliza Sara kwa umakini kama alivyo kuwa amemwambia, Yahwe akamfanyia Sara kama alivyo kuwa amemwahidi.
2 Sara akachukua mimba na akamzalia Abraham mtoto wa kiume katika uzee wake, katika muda ule ule ambao Mungu alikuwa amemwambia.
3 Abraham akamwita jina mwanawe, ambaye alizaliwa kwake, na Sara, Isaka.
4 Abraham akamtahiri mwanawe Isaka alipofikisha siku nane, kama vile Mungu alivyokuwa amemwagiza.
5 Abraham alikuwa na umri wa miaka mia moja wakati mwanawe Isaka anazaliwa kwake.
6 Sara akasema, “Mungu amenifanya nicheke; kila mtu atakaye sikia atacheka pamoja na nami.”
7 Pia akasema, “Nani angesema kwa Abraham kwamba Sara atalea mtoto, na sasa kweli nimemzalia mtoto wakiume katika uzee wake!”
8 Mtoto akakua na akaachishwa kunyonya, na Abraham akafanya sherehe kubwa katika siku ambayo Isaka aliachishwa.
9 Sara akamwona mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alikuwa amezaliwa kwa Abraham, akidhihaki.
10 Kwa hiyo akamwambia Abraham, “Mfukuze huyu mwanamke huyu mtumwa pamoja na mtoto wake: kwa kuwa mtoto huyu wa mwanamke mtumwa hawezi kuwa mrithi pamoja na mwanangu Isaka.”
11 Jambo hili likamuhuzunisha sana Abraham kwa sababu ya mwanawe.
12 Lakini Mungu akamwambia Abraham, “Usihuzunike kwa sababu ya kijana huyu, na kwa sababu ya mwanamke huyu mtumwa wako. Sikiliza maneno asemayo Sara juu ya jambo hili, kwa sababu itakuwa kupitia Isaka kwamba uzao wako utaitwa.
13 Nitamfanya pia mtoto wa mjakazi kuwa taifa, kwa sababu ni uzao wako.”
14 Abraham akaamka asubuhi na mapema, akachukua mkate na kiriba cha maji, akampatia Hajiri, akiweka juu ya bega lake. Akamtoa kijana akampatia Hajiri na akawaondoa. Hajiri akaondoka akapotea katika jangwa la Beerisheba.
15 Maji yalipokwisha kwenye kiriba akamtelekeza kijana katika moja ya vichaka.
16 Kisha akaondoka, na akakaa umbali kidogo na yule kijana, umbali kama wa kutupa mshale, kwa vile alisema, “Na nisitazame kifo cha mtoto.” Alipokuwa amekaa kumkabili, akapaza sauti yake akalia.
17 Mungu akasikia kilio cha kijana, na malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, “Nini kinakusumbua? Usiogope, kwa kuwa Mungu amesikia kilio cha kijana mahali alipo.
18 Inuka msimamishe mtoto, na umtie moyo; kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa.”
19 Kisha Mungu akayafunua macho ya Hajiri, natazama akaona kisima cha maji. Akaenda akajaza kiriba maji, na akampatia kijana akanywa.
20 Mungu akawa pamoja na kijana, na akakua. Akaishi jangwani akawa mwindaji.
21 Akaishi katka jangwa la Parani, na mama yake akampatia mke kutoka Misri.
22 Ikawa kwamba katika wakati ule Abimeleki na Fikoli kamanda wa jeshi lake akamwambia Abraham, akisema, “Mungu yuko pamoja na wewe katika yote uyatendayo.
23 Sasa niapie kwa Mungu kwamba hutanifanyia baya, wala mwanangu, wala uzao wangu. Onesha kwangu na kwa nchi ambayo umekuwa ukikaa agano lile lile la uaminifu ambalo nimekuonesha wewe.”
24 Abraham akasema, “Nina apa.”
25 Abraham pia akamlalamikia Abimeleki kuhusu kisima cha maji ambacho watumishi wa Abimeleki wamekinyang'anya.
26 Abimeleki akasema, “Sijui ni nani amefanya jambo hili. Hukuniambia mapema; na sijalisikia ila leo hii.”
27 Kwa hiyo Abraham akachukua kondoo na ng'ombe maksai akampatia Abimeleki, na wawili hawa wakafanya agano.
28 Kisha Abraham akatenga wanakondoo wa kike saba pekeyao.
29 Abimeleki akamwambia Abraham, “Nini maana ya hawa wanakondoo wa kike saba ambao umewatenga pekeyao?”
30 Akajibu, “Hawa wanakondoo wa kike saba utawapokea kutoka mkonono mwangu, ili kwamba uwe ushahidi kwangu, kuwa nichimba kisima hiki.”
31 Kwa hiyo akaita mahali pale Beerisheba, kwa sababu mahali pale wote wawili wali apa kiapo.
32 Walifanya agano hapo Bersheba, kisha Abimeleki na Fikoli, amiri wa jeshi, wakarudi katika nchi ya Wafilisti.
33 Abraham akapanda mti wa mkwaju katika Beerisheba. Na pale akamwabudu Yahwe, Mungu wa milele.
34 Abraham akasalia kuwa mgeni katika nchi ya Wafilisti kwa siku nyingi.