28
1 Isaka akamwita Yakobo, akambariki, na kumwagiza, “Usichukuwe mwanamke katika wanawake wa Kikanaani.
2 Inuka, nenda Padani Aramu, katika nyumba ya Bethueli baba wa mama yako, na uchukue mwanamke pale, mmojawapo wa binti za Labani, kaka wa mama yako.
3 Mungu Mwenyezi na akubariki, akupe uzao na akuzidishe, hata uwe wingi wa watu.
4 Na akupe baraka ya Ibrahimu, wewe, na uzao wako baada yako, kwamba uweze kumilki nchi ambapo umekuwa ukiishi, ambayo Mungu alimpa Ibrahimu.”
5 Hivyo Isaka akamwondoa Yakobo. Yakobo akaenda Padani Aramu, kwa Labani mwana wa Bethueli Mwaramu, kaka wa Rebeka, mama yao Yakobo na Esau.
6 Basi Esau alipoona kwamba Isaka amembariki Yakobo na kumpeleka Padani Aramu, kuchukua mke kutoka pale. Lakini pia akaona kwamba Isaka alikuwa amembariki na kumwagiza, akisema, “Usichukue mke katika wanawake wa Kanaani.”
7 Esau pia akaona kwamba Yakobo alikuwa amemtii baba yake na mama yake, na alikuwa amekwenda Padani Aramu.
8 Esau akaona kwamba wanawake wa Kanaani hawakumpendeza Isaka baba yake.
9 Hivyo akaenda kwa Ishmaeli, na kuchukua, mbali na wake aliokuwa nao, Mahalathi binti Ishmaeli, mwana wa Ibrahimu, dada wa Nebayothi, kuwa mke wake.
10 Yakobo akatoka Beersheba na akaelekea Harani.
11 Akaja mahali fulani na akakaa pale usiku kucha, kwa kuwa jua lilikuwa limekuchwa. Akachukua mojawapo ya mawe katika eneo hilo, akaliweka chini ya kichwa chake, na akalala usingizi katika eneo hilo.
12 Akaota na kuona ngazi imewekwa juu ya nchi. Ncha yake ilifika hata mbinguni na malaika wa Mungu walikuwa wakishuka na kupanda juu yake.
13 Tazama, Yahwe amesimama juu yake na kusema, “Mimi ni Yahwe, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka. Nchi uliyolala juu yake, nitakupa wewe na uzao wako.
14 Uzao wako utakuwa kama mavumbi ya ardhi, na utaenea mbali kuelekea magharibi, mashariki, kaskazini, na kusini. Kupitia kwako na kupitia uzao wako familia zote za dunia zitabarikiwa.
15 Tazama, mimi nipo nawe, na nitakulinda kila uendako, Nitakurudisha katika nchi hii tena; kwani sitakuacha. Nitafanya kila nililokuahidi.”
16 Yakobo akaamka katika usingizi, na akasema, “Hakika Yahwe yupo mahali hapa, sikujua hili.”
17 Akaogopa na kusema, “Eneo hili linatisha kama nini! Hili sio kingine zaidi ya nyumba ya Mungu. Hili ni lango la mbinguni.”
18 Yakobo akaamka mapema asubuhi na akachukua jiwe alilokuwa ameliweka chini ya kichwa chake. Akaliweka kama nguzo na kumimina mafuta juu yake.
19 Akapaita pale Betheli, lakini jina la kawaida la mji lilikuwa Luzu.
20 Yakobo akatoa nadhiri, kusema, “Ikiwa Mungu atakuwa nami na atanilinda katika njia nipitayo, na atanipa mkate wa kula, na mavazi ya kuvaa,
21 hata nikarudi salama katika nyumba ya baba yangu, ndipo Yahwe atakapokuwa Mungu wangu.
22 Kisha jiwe hili nililoliweka kama nguzo litakuwa jiwe takatifu. Kutoka katika kila utakachonipa, kwa hakika nitakupa tena sehemu ya kumi.”