41
1 Ikawa mwishoni mwa miaka miwili mizima Farao akaota ndoto.
2 Tazama, alikuwa amesimama kando ya Nile. Tazama, ng'ombe saba wakatoka katika mto Nile, wakupendeza na wanene, na wakajilisha katika nyasi.
3 Tazama, ng'ombe wengine saba wakatoka katika Nile baada yao, wasiopendeza na wamekondeana. Wakasimama ukingoni mwa mto kando ya wale ng'ombe wengine.
4 Kisha wale ng'ombe wasiopendeza na waliokonda wakawala wale waliokuwa wanapendeza na walionenepa.
5 Kisha Farao akaamka. Kisha akalala na kuota mara ya pili. Tazama, masuke saba ya nafaka yalichipua katika mche mmoja, mema na mazuri.
6 Tazama, masuke saba, membamba na yaliyokaushwa na upepo wa mashariki, yakachipua baada yake.
7 Masuke membamba yakayameza yale masuke saba mema yote. Farao akaamka, na, tazama, ilikuwa ni ndoto tu.
8 Ikawa wakati wa asubuhi roho yake ikafadhaika. Akatuma na kuwaita waganga na wenye hekima wote wa Misri. Farao akawasimlia ndoto zake, lakini hakuna aliyeweza kumtafsiria Farao.
9 Kisha mkuu wa wanyweshaji akamwambia Farao, “Leo ninayafikiri makosa yangu.
10 Farao aliwakasirikia watumishi wake, na kutuweka kifungoni katika nyumba ya kapteni wa walinzi, mkuu wa waokaji na mimi.
11 Tuliota ndoto usiku huo mmoja, yeye na mimi. Kila mmoja aliota kwa kadili ya tafsiri yake.
12 Pamoja nasi kulikuwa na kijana Mwebrania, mtumishi wa kapteni wa walinzi. Tulimwambia na akatutafsiria ndoto zetu. Alitutafsiria kila mmoja wetu kulingana na ndoto yake.
13 Ikawa kama alivyotutafsiria, ndivyo ilivyokuwa. Farao alinirudisha katika nafasi yangu, lakini akamtundika yule mwingine.”
14 Ndipo Farao alipotuma na kumwita Yusufu. Kwa haraka wakamtoa gerezani. Akajinyoa mwenyewe, akabadili mavazi yake, na akaingia kwa Farao.
15 Farao akamwambia Yusufu, “Nimeoda ndoto, lakini hakuna wa kuitafsiri. Lakini nimesikia kuhusu wewe, kwamba unaposikia ndoto unaweza kuitafsiri.”
16 Yusufu akamjibu Farao, kusema, “Siyo katika mimi. Mungu atamjibu Farao kwa uhakika.”
17 Farao akamwambia Yusufu, “Katika ndoto yangu, tazama, nilisimama katika ukingo wa Nile.
18 Tazama, ng'ombe saba wakatoka ndani ya Nile, wanene na wakuvutia, nao wakajilisha katika nyasi.
19 Tazama, ng'ombe wengine saba wakapanda baada yao, dhaifu, wabaya, na wembaba. Sijawao kuona wabaya kama hao katika nchi yote ya Misri.
20 Wale ng'ombe wembamba na wabaya wakawala wale ng'ombe saba na wanene.
21 Walipokuwa wamemaliza kuwala wote, haikujulikana kama walikuwa wamewala, kwani walibaki wabaya kama mwanzo. Kisha nikaamka.
22 Niliona katika ndoto yangu, na tazama, masuke saba yakatoka katika bua moja, jema na limejaa.
23 Tazama, masuke saba zaidi, yaliyonyauka, membamba na yamekaushwa na upepo wa mashariki, yakachipua baada yake.
24 Yale masuke membamba yakayameza masuke saba mema. Niliwaambia waganga ndoto hizi, lakini hakuna aliyeweza kunielezea.”
25 Yusufu akamwambia Farao, “Ndoto za Farao ni moja. Mungu amemwambia Farao kuhusu jambo analokwenda kulifanya.
26 Wale ng'ombe saba wema ni miaka saba, na masuke saba mema ni miaka saba. Ndoto ni moja.
27 Na wale ng'ombe saba wembamba na wabaya waliokuja baadaye ni miaka saba, na pia masuke saba membamba yaliyokaushwa na upepo wa mashariki itakuwa miaka saba ya njaa.
28 Hilo ni jambo nililomwambia Farao. Mungu amemfunulia Farao jambo analokwenda kulifanya.
29 Tazama, miaka saba yenye utele mwingi inakuja katika nchi yote ya Misri.
30 Na miaka saba ya njaa itakuja baada yake, na utele wote katika nchi ya Misri utasahaulika, na njaa itaiaribu nchi.
31 Utele hautakumbukwa katika nchi kwa sababu ya njaa itakayofuata, kwa kuwa itakuwa kali sana.
32 Kwamb ndoto ilijirudia kwa Farao sababu ni kwamba jambo hili limeanzishwa na Mungu, na Mungu atalitimiza hivi karibuni.
33 Basi Farao atafute mtu mwenye maharifa na busara, na kumweka juu ya nchi ya Misri.
34 Farao na afanye hivi: achague wasimamizi juu ya nchi. Na wachukue sehemu ya tano ya mazao ya Misri katika miaka saba ya shibe.
35 Na wakusanye chakula chote cha hii miaka myema ijayo na kuitunza nafaka chini ya mamlaka ya Farao, kwa chakula kutumika katika miji. Wakiifadhi.
36 Chakula kitakuwa matumizi ya nchi kwa miaka saba ya njaa itakayokuwa katika nchi ya Misri. Kwa njia hii nchi haitaaribiwa na njaa.”
37 Ushauri huu ukawa mwema machoni pa Farao na machoni pa watumishi wake wote.
38 Farao akawambia watumishi wake, “Je tunaweza kumpata mtu kama huyu, ambaye ndani yake kuna Roho wa Mungu?”
39 Hivyo Farao akamwambia Yusufu, “Kwa vile Mungu amekuonesha yote haya, hakuna mtu mwenye ufahamu na busara kama wewe.
40 Utakuwa juu ya nyumba yangu, watu wangu watatawaliwa kwa kadili ya neno lako. Katika kiti cha enzi peke yake mimi nitakuwa mkuu kuliko wewe.”
41 Farao akamwambia Yusufu, “Tazama, nimekuweka juu ya nchi yote ya Misri.”
42 Farao akavua pete yake ya mhuri kutoka katika mkono wake na kuiweka katika mkono wa Yusufu. Akamvika kwa mavazi ya kitani safi, na kuweka mkufu wa dhahabu shingoni mwake.
43 Akataka apandishwe katika kibandawazi cha pili alichokuwa nacho. Watu wakapiga kelele mbele yake, “Pigeni magoti.” Farao akamweka juu ya nchi yote ya Misri.
44 Farao akamwambia Yusufu, “Mimi ni Farao, mbali na wewe, hakuna mtu atakayeinua mkono wake au mguu wake katika nchi ya Misri.”
45 Farao akamwita Yusufu jina la Zafenathi Panea.” Akampa Asenathi, binti wa Potifera kuhani wa On, kuwa mke wake. Yusufu akaenda juu ya nchi yote ya Misri.
46 Yusufu alikuwa na umri wa miaka thelathini aliposimama mbele ya Farao, mfalme wa Misri. Yusufu akatoka mbele ya Farao, na kwenda katika nchi yote ya Misri.
47 Katika miaka saba ya shibe nchi ilipozaa kwa wingi.
48 Akakusanya chakula chote cha miaka saba iliyokuwako katika nchi ya Misri na kukiweka chakula katika miji. Akaweka katika kila mji chakula cha mashamba yaliyokizunguka.
49 Yusufu akahifadhi nafaka kama mchanga wa bahari, kingi kiasi kwamba akaacha kuhesabu, kwa sababu kilikuwa hakihesabiki.
50 Kabla miaka ya njaa kuingia Yusufu akapata wana wawili, ambao Asenathi, binti wa Potifera kuhani wa On, alimzalia.
51 Yusufu akamwita mzaliwa wake wa kwanza Manase, kwani alisema, “Mungu amenisahaurisha shida zangu zote na nyumba yote ya baba yangu.”
52 Akamwita mwanawe wa pili Efraimu, kwani alisema, Mungu amenipa uzao katika nchi ya mateso yangu.”
53 Miaka saba ya shibe iliyokuwa katika nchi ya Misri ikafika mwisho.
54 Miaka saba ya njaa ikaanza, kama alivyokuwa amesema Yusufu. Kulikuwa na njaa katika nchi zote, lakini katika nchi yote ya Misri kulikuwa na chakula.
55 Nchi yote ya Misri ilipokuwa na njaa, watu wakapiga kelele kwa Farao kwa ajili ya chakula. Farao akawambia Wamisri wote, “Nendeni kwa Yusufu na mfanye atakavyosema.”
56 Njaa ilikuwa juu ya uso wote wa nchi. Yusufu akafungua ghala zote na kuuza chakula kwa Wamisri. Njaa ilikuwa kali sana katika nchi ya Misri.
57 Dunia yote ikaja Misri kununua nafaka kutoka kwa Yusufu, kwani njaa ilikuwa kali katika dunia yote.