7
Na baada ya mambo haya Yesu alisafiri hivi katika Galilaya, kwa sababu hakupenda kwenda Uyahudi kwa sababu wayahudi walikuwa wakifanya mipango ya kumwua. Sasa sikukuu ya Wayahudi, sikukuu ya Vibanda, ilikuwa karibu. Ndipo ndugu zake walipomwambia, “Ondoka mahali hapa uende Uyahudi, ili kwamba wanafunzi wako vile vile wayaone matendo ufanyayo. Hakuna afanyaye lolote kwa siri iwapo yeye mwenyewe anataka kujulikana wazi. Iwapo unafanya mambo haya, jionyeshe mwenyewe kwa ulimwengu.” Hata ndugu zake pia hawakumwamini. Ndipo Yesu alipowaambia, “Wakati wangu haujafika bado, lakini wakati wenu kila mara uko tayari. Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi, bali unanichukia mimi kwa sababu ninaushuhudia kuwa matendo yake ni maovu. Pandeni kwenda katika sikukuu; mimi siendi katika sikukuu hii kwa sababu muda wangu haujakamilika bado.” Baada ya kusema mambo hayo kwao, alibaki Galilaya. 10 Hata hivyo, ndugu zake walipokuwa wamekwenda katika sikukuu, ndipo naye alienda, siyo kwa wazi bali kwa siri. 11 Wayahudi walikuwa wakimtafuta katika sikukuu na kusema, “Yuko wapi?” 12 Kulikuwa na majadiliano mengi miongoni mwa makutano juu yake. Wengine walisema, “Ni mtu mwema.” Wengine walisema, “Hapana, huwapotosha makutano.” 13 Hata hivyo hakuna aliyezungumza wazi juu yake kwa kuwaogopa Wayahudi. 14 Wakati sikukuu ilipofika katikati, Yesu alipanda kwenda Hekaluni na kuanza kufundisha. 15 Wayahudi walikuwa wakishangaa na kusema, “Kwa jinsi gani mtu huyu anajua mambo mengi? Hajasoma kamwe.” 16 Yesu akawajibu na kuwaambia, “Mafundisho yangu siyo yangu, bali ni yake yeye aliyenituma. 17 Iwapo yeyote atapenda kufanya mapenzi yake yeye, atajua kuhusu mafundisho haya, kama yanatoka kwa Mungu, au kama ninazungumza kutoka kwangu mwenyewe. 18 Kila anayezungumza yatokayo kwake mwenywe hutafuta utukufu wake, bali kila atafutaye utukufu wake yeye aliyemtuma, mtu huyo ni wa kweli, na ndani yake hakuna kutotenda haki. 19 Musa hakuwapa nyinyi sheria? Lakini hakuna hata mmoja kati yenu atendaye sheria. Kwa nini mnataka kuniua? 20 Makutano wakajibu, “Una pepo. Nani anataka kukuua?” 21 Yesu akajibu na akawaambia, “Nimetenda kazi moja, nanyi nyote mmeshangazwa kwa sababu yake. 22 Musa aliwapa tohara (siyo kwamba inatoka kwa Musa, bali ile inatoka kwa mababa), na katika Sabato mnamtahili mtu. 23 Iwapo mtu atapokea tohara katika siku ya Sabato ili kwamba sheria ya Musa isivunjwe, kwa nini mnanikasirikia mimi kwa sababu nimemfanya mtu kuwa mzima kabisa katika Sabato? 24 Msihukumu kulingana na mwonekano, bali hukumuni kwa haki. 25 Baadhi yao kutoka Yerusalemu wakasema, “Siye huyu wanayemtafuta kumwua? 26 Na tazama, anaongea wazi wazi, na hawasemi chochote juu yake. Haiwezi ikawa kwamba viongozi wanajua kweli kuwa huyu ni Kristo, inaweza kuwa? 27 Tunajua huyu mtu anatokea wapi. Kristo atakapokuja, hata hivyo, hakuna atakayejua wapi anakotoka.” 28 Yesu alikuwa akipaza sauti yake hekaluni, akifundisha na kusema, “Ninyi nyote mnanijua mimi na mnajua nitokako. Sikuja kwa nafsi yangu, bali yeye aliyenituma ni wa kweli, na hamumjui yeye. 29 Ninamjua yeye kwa sababu nimetoka kwake na alinituma.” 30 Walikuwa wanajaribu kumkamata, lakini hakuna hata mmoja aliyeinua mkono wake juu yake kwa sababu saa yake ilikuwa bado haijafika. 31 Hata hivyo, wengi katika makutano walimwamini. Walisema, “Kristo atakapokuja, atafanya ishara nyingi kuliko alizofanya mtu huyu?” 32 Mafarisayo waliwasikia makutano wakinong'onezana mambo haya kuhusu Yesu, na wakuu wa makuhani na Mafarisayo wakatuma maafisa ili kumkamata. 33 Ndipo Yesu aliposema, “Bado kuna muda kitambo niko pamoja nanyi, na baadaye nitakwenda kwake yeye aliyenituma. 34 Mtanitafuta wala hamtaniona; kule niendako, hamtaweza kuja.” 35 Kwa hiyo Wayahudi wakasemezana wao kwa wao, “Mtu huyu atakwenda wapi kwamba tusiweze kumuona? Ataenda kwa Waliotawanyika kati ya Wayunani na kuwafundisha Wayunani? 36 Ni neno gani hili alilolisema, 'Mtanitafuta wala hamtaniona; kule niendako hamtamweza kuja'?” 37 Sasa katika siku ya mwisho, siku kubwa ya sikukuu, Yesu alisimama akapaza sauti, akisema, “Ikiwa yeyote ana kiu, na aje kwangu anywe. 38 Yeye aniaminiye mimi, kama maandiko yalivyosema, kutoka ndani yake itatiririka mito ya maji ya uzima.” 39 Lakini aliyasema haya kuhusu Roho, ambaye wao wamwaminio watampokea; Roho alikuwa bado hajatolewa kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa bado. 40 Baadhi ya makutano, waliposikia maneno haya, walisema, “Kweli huyu ni nabii.” 41 Wengine walisema, “Huyu ni Kristo.” Lakini wengine walisema, “nini, Kristo aweza kutoka Galilaya? 42 Maandiko hayajasema kuwa Kristo atatokea katika ukoo wa Daudi na kutoka Bethlehemu, kijiji ambacho Daudi alikuwa? 43 Hivyo, pale ukainuka mgawanyiko katikati ya makutano kwa ajili yake. 44 Wengine kati yao wangelimkamata, lakini hakuna aliyenyoosha mikono yake juu yake. 45 Ndipo wale maofisa wakarudi kwa wakuu wa makuhani na Mafarisayo, nao wakawaambia, “Kwa nini hamjamleta?” 46 Maofisa wakajibu, “Hakuna mtu aliyewahi kuzungumza kama huyu kabla.” 47 Ndipo Mafarisayo walipowajibu, “Na nyinyi pia mmepotoshwa? 48 Kuna yeyote kati ya watawala anayemwamini, au yeyote wa Mafarisayo? 49 Bali hawa makutano wasiojua sheria - wamelaaniwa.” 50 Nikodemo akawaambia (yeye aliyemwendea Yesu zamani, akiwa mmoja wa Mafarisayo), 51 “Je sheria yetu inamhukumu mtu isipokuwa amesikilizwa kwanza na kujua anachokifanya?” 52 Walijibu na kumwambia, “Na wewe pia unatokea Galilaya? Tafuta na uone kwamba hakuna nabii aliyetokea Galilaya.” 53 (Zingatia: Baadhi ya maneno ya Yohana 7: 53 - 8: 11 hayamo katika nakala bora za kale). Kisha kila mtu alienda nyumbani kwake.