51
1 Yahwe asema hivi: Tazama, ninakwenda kuleta upepo wa maangamizi dhidi ya Babeli na dhidi yao waishio ndani ya Leb Kamei.
2 Nitawatuma Babeli wageni. Watamtawanya na wataifanya ukiwa nchi yake, maana watakuja kinyume chake kutoka pote siku ya madhara.
3 Msiwaache wapiga mishale wakapinda pinde zao; msiwache wakavaa silaha zao. Msiwahifadhi vijana wake wa kiume; litengeni jeshi lake lote kwa maangamizi.
4 Maana watu waliojeruhiwa wataanguka katika nchi ya Wakaldayo; waliouawa wataanguka katika mitaa yake.
5 Maana Israeli na Yuda hawajaachwa na Mungu wao, na Yahwe wa majeshi, japokuwa nchi yao imejaa na maasi yaliyotendwa kinyume cha Mmoja aliye Mtakatifu wa Israeli.
6 Kimbieni kutoka Babeli; kila mtu na ajiokoe mwenyewe. Msiangamie katika maasi yake. Maana ni wakati wa kisasi cha Yahwe. Atamlipa kwa yote.
7 Babeli alikuwa kikombe cha dhahabu mkononi mwa Yahwe kilichoinywesha nchi yote; mataifa walikunywa mvinyo wake wakawa wendawazimu.
8 Babeli utaanguka ghafla na kuangamizwa. Mwombolezeeni! mpeni dawa kwa maumivu yake; pengine aweza kupona.
9 Tulinuia kumponya Babeli, lakini hajaponywa, haya na tumwache twende, katika nchi yetu. Maana hatia yake imefika juu mbinguni; imerundikwa kufika mawinguni.
10 Yahwe ametamka kwamba sisi hatuna hatia. Njooni, teseme katika Sayuni matendo ya Yahwe Mungu wetu.'
11 Noweni mishale na kuchukua ngao. Yahwe anaiimiza roho ya mfalme wa Umedi katika mpango wa kuiangamiza Babeli. Hii ni kwa kisasi cha Yahwe, kisasi kwa maangamizi ya hekalu lake.
12 Inueni bendela juu ya kuta za Babeli; wekeni walinzi. Wekeni waangalizi; wekeni askari waviziao ili kumkamata kila akimbiliaye mjini, maana Yahwe atafanya kile alichokipanga. Atafanya alichokisema juu ya wakaao Babeli.
13 Enyi mwishio kati ya chemchemi nyingi za maji, ninyi mlio na wingi wa hazina, mwisho wenu umefika. upindo wa maisha yenu umepunguzwa.
14 Yahwe wa majeshi ameapa kwa maisha yake, 'nitakujaza na adui zako, kama pigo la nzige; watainua kelele za vita juu yako.'
15 Ameifanya dunia kwa nguvu zake; akaiweka dunia mahali kwa hekima yake. Kwa ufahamu wake alizitanda mbingu.
16 Anapovuma, kunakuwa na mvumo wa maji mbinguni, maana huleta umande kutoka miisho ya dunia. Hufanya radi kwa ajili ya mvua na kuituma na kuutuma upepo kutoka katika maghala ya nyumba zake.
17 Kila mtu anakuwa kama mnyama asiye na akili; kila mfua chuma ameaibishwa na sanamu zake. Maana mwonekano wake unadanganya; maana hakuna uzima ndani yake.
18 Hazifai, kazi ya wafanya mzaa; wataangamizwa wakati wa kuadhibiwa kwao.
19 Lakini Mungu, urithi wa Yakobo, siyo kama hawa, maana yeye ndiye afanyaye vitu vyote. Israeli ni kabila ya urithi wake; Yahwe wa majeshi ni jina lake.
20 Wewe ni nyundo ya vita yao, silaha ya vita yangu. Kwa wewe nitawaponda mataifa na kuharibu falme.
21 Kwa wewe nitaponda farasi na wawapandao; kwa wewe nitaponda vibandawazi na madereva wake.
22 Kwa wewe nitawafutilia mbali mme na mke; kwa wewe nitafutilia mbali mzee na kijana. Kwa wewe nitafutilia mbali kijana wa kiume na wasichana bikra.
23 Kwa wewe nitafutilia mbali wachungaji na makundi yao; kwa wewe nitawafutilia mbali wakulima na jozi zao za kulimia. kwa wewe nitawafutilia mbali watawala na maafsa.
24 Maana mbele yako nitamlipa Babeli na wote wakaao Ukaldayo kwa maovu yote waliyoyafanya huko Sayuni - hili ni tamko la Yahwe.
25 Tazama, mimi ni kinyume chako, ewe mlima, wewe unayewaharibu watu wengine - hili ni tamko la Yahwe - kuiharibu dunia yote. Nitakupiga na mikono yangu na kuvingirisha chini kutoka ukingo wa kilima. Kisha nitakufanya mlima ulioteketezwa kabisa kwa moto.
26 Hivyo hawatachukua kwako jiwe lolote ili kujengea pembe ya nyumba au msingi; kwani utakuwa ukiwa wa milele - hili ni tamko la Yahwe.
27 Inua bendela ya vita juu ya nchi. Piga tarumbeta katika mataifa. Yaite mataifa yamshambuliye: Ararati, Mini na Ashkenazi. Teua majemedari wa kumshambulia; leta farasi kama nzige warukao.
28 Waandae mataifa kumshambulia: wafalme wa Umedi na magavana wao, maafsa wake wote na nchi yake yete.
29 Maana nchi itatikisika na kudhoofika, kwa kuwa mipango ya Yahwe inaendelea juu ya Babeli, kuifanya nchi ya Babeli kuwa nchi isiyofaa mahali pasipo na mtu.
30 Maaskari wameacha kupigana huko Babeli; wamekaa katika ngome zao. Nguvu zao zimeshindwa; wamekuwa wanawake - nyumba zake zipo motoni, makomeo ya malango yake yamevunjika.
31 Mjumbe hukimbia ili amwambie mjumbe mwingine, na mtoa habari humwambia mtoa habari mwingine ili amwambie mfalme wa Babeli kwamba mji wake umetwaliwa kutoka mwisho hata mwisho.
32 Hivyo vivuko katika mito vimekamatwa; adui anaunguza mafunjo ya bwawa, na wapiganaji wa Babeli wamechanganyikiwa.
33 Maana Yahwe wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: Binti Babeli ni kama sakafu ya kupuria. Ni muda wa kumkanyaga. Ni kitambo kidogo wakati wa mavuno utakuja juu yake.
34 Yerusalemu husema, 'Nebukadneza mfalme wa Babeli amenirarua. Amenikausha na amenifanya kuwa mtungi mtupu. Amenimeza kama joka. Alijishibisha kwa chakula changu chema. Amenitupa mbali.'
35 Wenyeji wa Sayuni watasema, 'Gasia nilizofanyiwa na mwili wangu na ziwe kwa Babeli.' Yerusalem atasema, Damu yangu na iwe juu ya wakaao Ukaldayo.'
36 Kwa hiyo Yahwe asema hivi: Tazama, nikotayari kulitetea shitaka lako na kuleta kisasi kwa ajili yako. Maana nitayakausha maji ya Babeli na kufanya vyanzo vyake kukauka.
37 Babeli utakuwa rundo la magofu, pango la mbwea, sehemu itishayo, kitu cha kutoa sauti ya nyoka, pasipo na watu.
38 Wababeli wataunguruma kwa pamoja kama wanasimba. Watanguruma kama watoto wa simba.
39 wanapopashwa moto kwa hasira, nitawafanyia sherehe; nitawalewesha hata wafurahi, na kisha kulala usingizi usio na mwisho hata wasiamke - hili ni tamko la Yahwe -
40 nitawapeleka chini kama wanakondoo kwa mchinjaji, kama kondoo dume pamoja na mbuzi majike.
41 Jinsi Babeli ulivyotekwa! Hivyo fahari ya dunia yote imekamatwa. Jinsi Babeli ulivyofanyika sehemu yenye magofu kati ya mataifa.
42 Bahari imekuja juu ya Babeli! Amefunikwa na mawimbi yavumayo.
43 Miji yake imekuwa ukiwa, sehemu kame na nyika, nchi isiyo na watu, na hakuna mtu apitaye hapo.
44 Hivyo nitamwadhibu Beli huko Babeli; nitakitoa kinywani mwake alichokimeza, na mataifa hawatamminikia tena pamoja na wazao wao. Kuta za Babeli zitaanguka.
45 Tokeni kati yake, enyi watu wangu. Kila mmoja wenu aokowe maisha yake kutoka katika hasira ya gadhabu yangu.
46 Msiache mioyo yenu ikaogopa au kuhofu habari iliyosikiwa nchini, maana habari itakuja siku moja. Baada yake mwaka unaofuata kutakuwa na habari, na ghasia zitakuwa nchini. Mtawala atakuwa kinyume cha mtawala.
47 Kwa hiyo, tazama, siku zinakuja nitakapoadhibu sanamu za Babeli. Nchi yake yote itaaibika, na wote waliochinjwa wataanguka ndani yake.
48 Kisha mbingu na nchi, na vyote vilivyomo ndani yake vitafurahi juu ya Babeli. Maana mwalibifu atamwijia kutoka kaskazini - hili ni tamko la Yahwe.
49 “Kama Babeli alivyowafanya waliouawa wa Israeli kuanguka, hivyo waliouawa katika nchi yake wataanguka katika Babeli.
50 Ondokeni!, manusura wa vita, Msikawiye. Mkumbukeni Yahwe tokea mbali; Yerusalemu na ikumbukwe.
51 Tumeaibika, maana tumesikia matusi; dhihaka imefunika nyuso zetu, maana wageni wameingia mahali patakatifu pa nyumba ya Yahwe.
52 Kwa hiyo, tazama, siku zinakuja - hivi ndivyo asemavyo Yahwe - nitakapoziadhibu sanamu zake, na waliojeruhiwa watanung'unika kwa maumivu katika nchi yake yote.
53 Maana hata kama Babeli angepanda mbinguni au kujenga ngome zake ndefu, aharibuye kutoka kwangu angemwendea - hili ni tamko la Yahwe.
54 Kelele ya maangamizi ilitoka Babeli, anguko kubwa kutoka nchi ya Wakaldayo.
55 Maana Yahwe anaiharibu Babeli. Anaifanya kelele ya sauti yake kuisha. Adui zake wanaunguruma kama mawimbi ya maji mengi; kelele yao imekuwa na nguvu.
56 Maana aharibuye amekuja kinyume chake - kinyume cha Babeli! - na shujaa wake wametekwa. Pinde zao zimevunjwa, maana Yahwe ni Mungu wa kisasi; atatekeleza kisasi hiki.
57 Maana nitawafanya wana wafalme wake, wenye hekima wake, maofsa wake, na maaskari wake kulewa, nao watalala usingizi kwa usingizi usioisha na bila kuamka - hili ni tamko la mfalme: Yahwe wa majeshi ndilo jina lake.
58 Yahwe wa majeshi asema hivi: Ukuta mnene wa Babeli utaangushwa kabisa, na malango marefu yataunguzwa. Kisha watu wanaokuja kumsaidia watafanya kazi isiyofaa; kila mataifa wanachojaribu kikifanya kwa ajili yake kitateketezwa kwa moto.”
59 Hili ndilo neno Yeremia nabii alilomwamru Seraya mwana wa Neria mwana wa Makseya alipokwenda na Sedekia mfalme wa Yuda huko Babeli katika mwaka wa nne wa kutawala kwake. Basi Seraya alikuwa afsa mwandamizi.
60 Maana Yeremia alikuwa ameandika katika gombo kuhusu madhara yote yeliyokuwa yakienda kutendeka juu ya Babeli - maneno haya yote yaliyokuwa yameandikwa juu ya Babeli
61 Yeremia akamwambia Seraya, “Unapokwenda Babeli, hakikisha unayasoma maneno haya yote.
62 Nawe utasema, 'Yahwe, wewe! - wewe mwenyewe umesema kwamba utapaharibu mahali hapa. Hapatakuwa na wa kukaa, kwamba ni watu au wanyama. Patakuwa nchi isiyofaa daima.'
63 Kisha mtakapomaliza kusoma gombo hili, funga jiwe kubwa juu yake na ulitupe katikati ya Frati.
64 Sema, 'Babeli utazama kama hivi. Hautainuka kwa sababu ya mabaya ninayoyapeleka juu yake, nao wataanguka.” Maneno ya Yeremia yanaishia hapa.