17
1 Na huu ndio mgao wa nchi kwa ajili ya kabila la Manase (aliyekuwa mzaliwa wa kwanza wa Yusufu), ambayo ilikuwa kwa ajili ya Makiri, mzaliwa wa kwanza wa Manase, ambaye alikuwa ni baba wa Gilieadi. Watoto wa Makiri walipewa nchi ya Gileadi na Bashani, kwasababu Makiri alikuwa ni mtu wa vita.
2 Nchi iliyobaki iligawiwa kwa kabila la Manase, walipewa kwa koo zao, ambazo ni Abi Ezeri, Heleki, Asrieli, Shekemu, Heferi, na Shemida. Hawa walikuwa ni watoto wa kiume wa Manase mwana wa Yusufu, waliwakilishwa na koo zao.
3 Basi Zelofehadi mwana wa Heferi mwana wa Gileadi mwana wa Makiri mwana wa Manase hakuwa na watoto wa kiume, bali alikuwa na watoto wa kike tu. Na majina ya binti zake yalikuwa Mahila, Noa, Hogla, Milka na Tirsa.
4 Walimwendea Eliazeri kuhani, Yoshua mwana wa Nuni, na viongozi na wakasema, “Yahweh alimwagiza Musa atupatie urithi wetu pamoja na kaka zetu.” Hivyo, kwa kuzingatia agizo la Yahweh, aliwapa wanawake hao urithi miongoni mwa ndugu za baba yao.
5 Manase alipewa sehemu kumi za nchi katika Gileadi na Bashani, ambayo iko upande mwingine wa Yordani,
6 kwasababu ya binti za Manase walipokea urithi pamona na watoto wake wa kiume. Nchi ya Gileadi iligawanywa kwa kabila la Manase lililosalia.
7 Eneo la Manase lilianzia Asheri hadi Mikimethathi, ambayo iko mashariki mwa Shekemu. Kisha mpaka ulienda upande wa kusini kwa wale walioishi karibu na chemichemi ya Tapua.
8 ( Nchi ya Tapua ilikuwa ni miliki ya Manase, lakini mji wa Tapua katika mpaka wa Manase ilikuwa ni mali ya kabila la Efraimu.)
9 Kisha mpaka ulishuka kuelekea kijito cha Kana. Miji hii kusini mwa kijito miongoni mwa miji ya Manase ilikuwa ni mali ya Efraimu. Mpaka wa Manase ulikuwa upande wa kaskazini wa kijito, na ulikomea katika
10 bahari. Na nchi iliyokuwa upande wa kusini ilikuwa ni ya Efraimu, na nchi iliyo upande wa Kasikazini ilikuwa ni ya Manase; bahari ilikuwa ndoi mpaka. Kwa upande wa kaskazini ulifika hata Asheri, na upande wa mashariki, Isakari.
11 Pia katika Isakari na katika Asheri, Manase alimiliki Bethi Shani na vijiji vyake, Ibleamu na vijiji vyake, wenyeji wa Dori na vijiji vyake, wenyeji wa Endori na vijiji vyake, wenyeji wa Taanaki na vijiji vyake, na wenyeji wa Megido na vijiji vyake (na mji wa tatu ni Nafethi).
12 Lakini kabila la Manase halikuweza kuimiliki miji hiyo, kwa kuwa Wakanaani waliendelea kuishi katika nchi hii.
13 Hata wakati watu wa Israeli walipopata nguvu zaidi, hawakuwafukuzia mbali kabisa Wakanaani, bali waliwafanya kuwa watumwa.
14 Kisha wazawa wa Yusufu wakamwambia Yoshua, wakisema, “ Kwanini umetupa mgao mmoja wa nchi na sehemu moja kwa ajili ya urithi, kwa kuwa tuko wengi, na kwa muda wote Yahweh umetubaliriki?
15 Yoshua akawaambia, “Kama ninyi ni watu wengi katika hesabu, pandeni ninyi wenyewe katika msitu na kuisafisha nchi kwa ajili yenu wenyewe katika nchi ya Waperizi na ya Refaimu. Fanyeni hivi kwa kuwa nchi ya milima ya Efraimu ni ndogo kwenu.”
16 Wazawa wa Yusufu wakasema, “Nchi ya milima haitutoshi. Lakini Wakanaani wote wanaoishi katika bonde wana magari ya chuma, wote walio katikaBethi Shani na vijiji vyake, na wale walio katika bonde la Yezreeli.”
17 Kisha Yoshua akawaambi nyumba ya Yusufu, ambao ni Efraimu na Manase, “ Ninyi ni watu mlio wengi katika hesabu, na mna nguvu kubwa. Hamtakiwi kuwa na sehemu moja ya nchi mliogawiwa.
18 Nchi ya milima itakuwa yenu pia. Ingawa ni msitu, mtaufyeka na kuimiliki hata mipaka yake ya mbali. Mtawafukuzia mbali Wakanaani, ingawa wanayo magari ya chuma na ingawa pia wanazo nguvu.”