12
1 Rehoboamu akaenda Shekemu, kwa kuwa Israeli yote walikuwa wameenda Shekemu kumfanya awe mfalme.
2 Ikatokea kuwa Yeroboamu mwana wa Nebati akayasikia haya (Kwa kuwa alikuwa bado yuko Misri, ambako alikuwa amekimbilia kumkwepa mfalme Sulemani), Kwani Yeroboamu alikuwa anaishi Misri.
3 Kwa hiyo wakatuma watu kumwita, na Yeroboamu pamoja na mkutano wote wa Israeli wakaja wakamwambia Rehoboamu,
4 Baba yako aliifanya nira yetu kuwa nzito. Sasa ifanye kazi ngumu ya baba yako kuwa nyepesi kuliko nira ngumu ambayo baba yako alituwekea, nasi tutakutumikia.”
5 Naye Rehobiamu akawaambia, “Ondokeni kwa siku tatu, kisha nirudieni.” Kwa hiyo watu wakaondoka.
6 Mfalme Rehoboamu akatafuta ushauri kwa wazee waliokuwa wamesimama mbele ya Sulemani baba yake wakati wa uhai wake, naye akasema, “mnanishauri niwajibuje hawa watu?”
7 Nao wakamwambia, “Kama wewe utakuwa mtumishi wa hawa watu na akawatumikia, na akawapa majibu ya maneno mema, ndipo watakapokuwa watumishi wako daima.”
8 Lakini Rehoboamu akapuuzia ushauri aliopewa na wazee na akaenda kuomba ushauri kwa vijana ambao alikua pamoja nao wakasimama mbele yake.
9 Akawaambia, “Mnanipa ushauri gani ili niweze kuwajibu hawa watu waliosema nami kwamba, 'ifanye nyepesi nira ambayo baba yako alituwekea'”
10 Wale vijana waliokua pamoja na Rehoboamu wakamjibu, wakisema, “Waambie hawa watu kuwa baba yako Sulemani aliifanya nira yenu kuwa nzito lakini ninyi wenyewe mnaweza kuifanya rahisi. Uwaambie hivi, 'Kidole changu kidogo ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu.
11 Kwa hiyo sasa, ingawa baba yangu aliwatwika kongwa zito, Mimi nitaiongeza kongwa lenu. Baba yangu aliwaadhibu kwa mijeredi, Lakini mimi nitawaadhibu kwa nge.'”
12 Kwa hiyo siku ya tatu Yeroboamu na watu wote wakaja kwa Rehoboamu, kama mfalme alivyokuwa amewaelekeza aliposema, “mrudi kwangu siku ya tatu.”
13 Naye mfalme akawaambia wale watu kwa ukali na akapuuzia ushauri wa wale wazee ule waliokuwa wamempatia.
14 Akawaambia akifuata ushauri wa wale vijana; akasema, “Baba yangu aliwatwika kongwa zito, lakini mimi nitaongeze kongwa lenu. Baba yangu aliwaadhibu kwa mijeredi, mimi nitawaadhibu kwa nge.”
15 Kwa hiyo mfalme hakuwasikiliza wale watu, kwa kuwa ilikuwa zamu ya tukio lililoletwa na BWANA, ili kwamba aweze kulitimiza neno lake ambalo alikuwa amelisema kupitia Ahiya.
16 Israeli yote ilipoona kuwa mfalme hakuwasikiliza, watu wakamjibu wakimwambia, “Je, tuna sehemu gani kwa Daudi? Hatuna urithi kwa mwana wa Yese! Nenda kwenye hema zako, ewe Israeli. Sasa tazama kwenye nyumba yako, Daudi.” Kwa hiyo Israeli akarudi kwenye hema zake.
17 Lakini kwa watu wa Israeli waliokuwa wakiishi kwenye miji ya Yuda, Rehoboamu akawa mfalme juu yao.
18 Kisha mfalme Rehoboamu akamtuma Adoramu, aliyekuwa juu ya shokoa, lakini Waisraeli wote wakampiga kwa mawe wakamwua kwa mawe. Mflme Rehoboamu akakimbia haraka kwa gari lake kwenda Yerusalemu.
19 Kwa hiyo Israeli wakawa wapinzani dhidi ya nyumba ya Daudi mpaka leo.
20 Ndipo Israeli yote waliposikia kuwa Yeroboamu alikuwa amerudi, walimwita kwenye kusanyiko lao wakamweka kuwa mfalme wa Israeli. Hapakuwepo na mtu aliyeifuata familia ya Daudi, isipokuwa tu kabila la Yuda.
21 Rehoboamu alipofika Yerusalemu, akawakusanya wote wa nyumba ya Yuda na kabila la Benjamini; walichaguliwa wanaume wanajeshi180, 000 ili wapigane na nyumba ya Israeli, kwa lengo la kurudisha ufalme kwa Rehoboamu mwana wa Sulemani.
22 Lakini neno la Mungu likamjia Shemaya, mtu wa Mungu; likisema,
23 “Mwambie Rehoboamu mwana wa Sulemani, mfalme wa Yuda, na kwa nuymba yote ya Yuda na Benjamini, na kwa watu wote; uwaambie,
24 “BWANA asema hivi, Usipigane wala kuwavamia ndugu zako watu wa Israeli. Kila mtu lazima arudi nyumbani kwake, kwa kuwa jambo hili nimelisababisha mimi.” Kwa hiyo wakalisikiliza neno la BWANA na wakrudi nyumbani kwa njia zao na wakalitii neno lake.
25 Kisha Yeroboamu akaijenga Shekemu katika nchi ya milima ya Efraimu, na akaishi huko. Akatoka huko na kuijenga Penueli.
26 Yeroboamu akafikiri moyoni mwake, “Sasa ufalme utarudi kwenye nyumba ya Daudi.
27 Kama hawa watu wataenda kutoa sadaka kwenye hekalu la BWANA kule Yerusalemu, basi mioyo ya hawa watu itarudi tena kwa bwana wao, kwa Rehoboamu mfalme wa Yuda. Wataniua na kurudi kwa Rehoboamu mfalme wa Yuda.”
28 Kwa hiyo mfalme Yeroboamu akatafuta ushauri na akafanya ndama wawili wa dhahabu; akawaambia watu, “Ni vigumu sana kwenu kwenda Yerusalemu. Tazameni, hawa ndiyo miungu yenu, Ee Israeli, iliyowatoa toka nchi ya Misri.”
29 Akamweka mmoja Betheli na mwingine Dani.
30 Kwa hiyo jambo hili likawa dhambi. Watu wakaenda kwa huyo na wengine kwa hawa, mpaka huko Dani.
31 Yeroboamu akajenga nyumba mahali pa juu na kufanya makuhani kutoka kwa watu wote, ambao hawakuwa wana wa Lawi.
32 Yeroboamu akafanya sikukuu katika mwezi wa nane, katika siku ya kumi na tano ya mwezi, kama sikukuu ambayo iko Yuda, na akaenda juu kwenye madhabahu. Akafanya hivyo kule Betheli, akawatolea sadaka wale ndama aliokuwa amewatengeneza, na akaweka kuhani huko Betheli mahali pa juu alipokuwa amepatengeneza.
33 Yeroboamu akapanda kwenda kwenye madhabahu ambayo aliitengeneza kule Betheli katika siku ya kumi na tano ya mwezi wa nane, ndio mwezi aliokuwa amefikiri katika akili yake; akafanya sikukuu kwa watu wa Israeli n a akaenda madhabahuni kufukiza uvumba.