19
1 Yesu aliingia na kupita katikati ya Yeriko.
2 Na hapo palikuwa na mtu mmoja aitwaye Zakayo. Ambaye alikuwa mkuu wa watoza ushuru tena mtu tajiri.
3 Alikuwa anajaribu kumwona Yesu ni mtu wa namna gani, lakini hakuweza kuona kwa sababu ya umati wa watu, kwa kuwa alikuwa mfupi wa kimo.
4 Hivyo, alitangulia mbio mbele za watu, akapanda juu ya mkuyu ili aweze kumwona, kwa sababu Yesu alikaribia kupita njia hiyo.
5 Wakati Yesu alipofika mahali pale, aliangalia juu akamwambia, 'Zakayo, shuka upesi, maana leo ni lazima nishinde nyumbani mwako.'
6 Akafanya haraka, akashuka na kumkaribisha kwa furaha.
7 Watu wote walipoona hayo, wakalalamika, wakisema, 'Amekwenda kumtembelea mtu mwenye dhambi.'
8 Zakayo akasimama akamwambia Bwana, Tazama Bwana nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimemnyang'anya mtu yeyote kitu, nitamrudishia mara nne. '
9 Yesu akamwambia, 'Leo wokovu umefika katika nyumba hii, kwa sababu yeye pia ni mwana wa Ibrahimu.
10 Kwa maana Mwana wa Mtu amekuja kutafuta na kuokoa watu waliopotea. '
11 Waliposikia hayo, aliendelea kuongea na alitoa mfano, kwa sababu alikuwa karibu na Yerusalemu, na wao walidhani ya kuwa ufalme wa Mungu ulikuwa karibu kuonekana mara moja.
12 Hivyo akawaambia, 'Ofisa mmoja alikwenda nchi ya mbali ili apokee ufalme na kisha aurudi.
13 Aliwaita watumishi wake kumi, akawapa mafungu kumi, akawaambia, 'fanyeni biashara mpaka nitakaporudi.'
14 Lakini wananchi wake walimchukia na hivyo wakatuma wajumbe waende kumfuata na kusema, 'Hatutaki mtu huyu atutawale.'
15 Ikawa aliporudi nyumbani baada ya kufanywa mfalme, akaamuru wale watumishi aliokuwa amewaachia fedha waitwe kwake, apate kujua faida gani waliyoipata kwa kufanya biashara.
16 Wa kwanza akaja, akasema, `Bwana, fungu lako limefanya mafungu kumi zaidi. '
17 Huyo Ofisa akamwambia, Vema, mtumishi mwema. Kwa sababu ulikuwa mwaminifu katika jambo dogo, utakuwa na madaraka juu ya miji kumi. '
18 Wa pili akaja, akasema, 'Bwana, fungu lako limefanya mafungu matano.'
19 Huyo Afisa akamwambia, 'Chukua mamlaka juu ya miji mitano.'
20 Na mwingine akaja, akasema, `Bwana hii hapa fedha yako, ambayo niliihifadhi salama katika kitambaa,
21 kwa maana niliogopa kwa sababu wewe ni mtu mkali. Unaondoa kile usichokiweka na kuvuna usichopanda. '
22 Huyo Ofisa akamwambia, 'Kwa maneno yako mwenyewe, nitakuhukumu, ewe mtumishi mbaya. Ulijua kwamba mimi ni mtu mkali, nachukua nisichokiweka na kuvuna ambacho sikupanda.
23 Basi, mbona hukuweka fedha yangu katika benki, ili nikirudi niichukue pamoja na faida?
24 Ofisa akawaambia watu waliokuwa wamesimama hapo, 'Mnyang'anyeni hilo fungu na kumpa yule mwenye mafungu kumi.'
25 Wakamwambia, `Bwana, yeye ana mafungu kumi. '
26 'Nawaambia, kila mtu ambaye anacho atapewa zaidi, lakini ambaye hana, hata kile alicho nacho kitachukuliwa.
27 Lakini hawa maadui zangu, ambao hawakutaka niwe Mfalme wao, waleteni hapa na kuwaua mbele yangu. ''
28 Baada ya kusema hayo, aliendelea mbele akipanda kwenda Yerusalemu.
29 Ikawa alipokaribia Bethfage na Bethania, karibu na mlima wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili,
30 akisema: `Nendeni katika kijiji cha jirani. Mkiingia, mtakuta mwana-punda hajapandwa bado. Mfungueni, mkamlete kwangu.
31 Kama mtu akiwauliza, `Mbona mnamfungua? ' Semeni, “Bwana anamhitaji. ''
32 Wale waliotumwa wakaenda wakamwona mwana-punda kama Yesu alivyokuwa amewaambia.
33 Walipokuwa wanamfungua mwana punda wamiliki wakawaambia, 'Kwa nini mnamfungua mwana punda huyu?'
34 Wakasema, `Bwana anamhitaji. '
35 Basi, wakampelekea Yesu, wakatandika nguo zao juu ya mwana punda na wakampandisha Yesu juu yake.
36 Alipokuwa akienda watu wakatandaza mavazi yao barabarani.
37 Alipokuwa anateremka mlima wa Mizeituni, jumuiya yote ya wanafunzi wakaanza kushangilia na kumtukuza Mungu kwa sauti kubwa, kwa sababu ya mambo makuu waliyoyaona,
38 wakisema, 'Ndiye mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana! Amani mbinguni, na utukufu juu!'
39 Baadhi ya Mafarisayo katika mkutano wakamwambia, Mwalimu, wanyamazishe wanafunzi wako. '
40 Yesu akajibu, akasema, `Nawaambieni, kama hawa wakinyamaza, mawe yatapaza sauti. '
41 Yesu alipoukaribia mji aliulilia,
42 akisema, laiti ungelijua hata wewe, katika siku hii mambo ambayo yanayokuletea amani! Lakini sasa yamefichika machoni pako.
43 Kwa kuwa siku zinakuja ambapo adui zako watajenga boma karibu na wewe, na kukuzunguka na kukukandamiza kutoka kila upande.
44 Watakuangusha chini wewe na watoto wako. Hawatakuachia hata jiwe moja juu ya jingine, kwa sababu haukutambua wakati Mungu alipokuwa anajaribu kukuokoa'.
45 Yesu aliingia Hekaluni, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakiuza,
46 akiwaambia, “Imeandikwa, 'Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala,' lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi”.
47 Kwa hiyo, Yesu alikuwa akifundisha kila siku hekaluni. Makuhani wakuu na walimu wa Sheria na viongozi wa watu walitaka kumuua,
48 lakini hawakuweza kupata njia ya kufanya hivyo, kwa sababu watu wote walikuwa wakimsikiliza kwa makini.