19
1 BWANA akanena na Musa na Haruni, Akasema,
2 “Hii ni amri, ni sheria ninayokuamuru: Waambie wana waIsraeli wakuletee ng'ombe mke mwekundu asiyekuwa na kipaku wala waa, ambaye hajawahi kubeba nira.
3 Mpatie Eliazari kuhani huyo ng'ombe jike. Naye atamtoa nje ya kambi, na mtu mmoja amchinje mbele yake.
4 Kisha Eliazari kuhani atachukua sehemu ya damu yake kwa kidole chake na kuinyunyiza mara saba akielekea sehemu ya mbele ya ile hema ya kukutania.
5 Na kuhani mwingine atamchoma huyo ng'ombe mbele ya macho yake. Ataichoma ngozi yake, nyama yake, na damu yake pamoja na mavi yake,
6 Yule kuhani atachukua mti wa mwerezi, na hisopo na sufu na kivitupa katikati ya huyo ng'ombe anayechomwa.
7 Kisha atazifua nguo zake na kuoga kwenye maji. Ndipo atakuja kambini, ambapo atabaki najisi mpaka jioni ya siku hiyo.
8 Yule aliyemchoma huyo ng'ombe mke atafua nguo zake kwa maji na kuoga majini. Naye atabaki najisi mpaka jioni ya siku ile.
9 Baadaye mtu aliyesafi atayakusanya hayo majivu ya ng'ombe huyo na kuyaweka nje ya kambi kwenye eneo safi. Majivu haya yatatunzwa kwa ajili ya jamii ya watu wa Israeli. Watayachanganya majivu na maji kwa ajili ya utakaso wa dhambi, kwa kuwa majivu yalitokana na sadaka ya dhambi.
10 Yule aliyeyakusanya majivu ya ng'ombe huyo lazima afue mavazi yake. Atabaki najisi mpaka jioni ya siku ile. Hii itakuwa sheria ya kudumu kwa watu wa Israeli na kwa wageni wanaoishi nao.
11 Yeyote atakayegusa maiti ya mtu atakuwa najisi kwa siku saba.
12 Mtu wa jinsi hiyo atajitakasa mwenyewe siku ya tatu na siku ya saba. Ndipo atakapokuwa safi. Lakini kama hatajitakasa mwenyewe katika siku ya tatu, basi hatakuwa safi siku ya saba.
13 Yeyote atakayegusa mtu aliyekufa, maiti ya mtu aliyekufa na hajajitakasa - mtu huyu anainajisi masikani ya BWANA. Mtu huyo ataondolewa kuwa miongoni mwa Waisraeli kwa sababu maji ya farakano hayakunyunyiziwa kwake. Atabaki najisi; na unajisi wake utabaki kwake.
14 Hii ndiyo sheri ya mtu anayefia hemani. Kila mtu aingiaye hemani na kila mtu ambaye tayari yumo hemani atakuwa najisi kwa siku saba.
15 Kila chombo ambacho hakina kifuniko kinanajisika.
16 Vivyo hivyo, kwa mtu aliye nje ya hema ambaye atamgusa mtu aliyeuawa kwa upanga, au mzoga wowote, au mfupa wa mtu, au kaburi—mtu huyo atakuwa najisi kwa siku saba.
17 Fanyeni hivi kwa mtu najisi: twaeni majivu ya sadaka ya dhaambi ya kuteketezwa na myacahanganye kwenye chombo chenye maji ya mto.
18 Ndipo mtu aliye safi atachukua hisopo, na kutia katika hayo maji, na kunyunyizia juu ya hema, na katika vyombo vyote vilivyo hemani, na kwa watu waliokuwepo, na kwa yule aliyegusa ule mfupa, mtu aliyeuawa, maiti, au kaburi.
19 Katika siku ya tatu na siku ya saba, yule mtu aliye msafi atamnyunyizia yule mtu asiyekuwa safi. Katika siku ya saba mtu najisi atajitakasa mwenyewe. Atazifua nguo zake na kuoga kwenye maji. Jioni yake atakuwa safi.
20 Lakini yule atakayebaki najisi, anayekataa kujitakasa mwenyewe — huyo mtu ataondolewa kutoka kwenye jamii, kwa sababu amepanajisi patakatifu pa BWANA. Hajanyunyiziwa maji ya utakaso; atabaki najisi.
21 Hii itakuwa sheria ya kudumu kuhusiana na hali ya hivi. Yule mtu anayenyunyizia maji ya farakano atafua mavazi yake. Yule atakayeyagusa maji ya farakano atakuwa najisi mpaka jioni.
22 Chochote kile ambacho kitaguswa na mtu najisi kitakuwa najisi. na mtu atakayekigusa naye atakuwa najisi mpaka jioni.