Wafilipi
1
1 Paulo na Timotheo, watumishi wa Kristo Yesu, Kwa wale walitengwa katika Kristo wanaoishi Filipi, pamoja na waangalizi na mashemasi.
2 Neema na iwe kwenu na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo.
3 Namshukuru Mungu wangu kila ninapowakumbuka ninyi nyote.
4 Mara zote katika kila ombi langu kwa ajili yenu ninyi nyote, huwa na furahi ninapowaombea.
5 Nina shukrani nyingi kwa sababu ya ushirika wenu katika injili tangu siku ya kwanza mpaka leo.
6 Nina hakika kuwa yeye aliyeanzisha kazi njema ndani yenu ataendelea kuikamilisha mpaka siku ya Bwana Yesu Kristo.
7 Ni sawa kwangu kujisikia hivi juu yenu ninyi nyote kwa sababu nimewaweka moyoni wangu. Maana ninyi mmekuwa washirika wenza katika neema katika kifungo changu na katika utetezi na uthibitishaji wangu wa injili.
8 Mungu ni shahidi wangu, jinsi nilivyo na shauku juu ya yenu nyote katika undani wa pendo la Kristo Yesu.
9 Na ninaomba kwamba: upendo wenu uongezeke zaidi na zaidi katika maarifa na ufahamu wote.
10 Ninaomba kwa ajili ya hili ili muwe na uwezo wa kupima na kuchagua mambo yaliyo bora sana. Pia ninawaombea ili muwe safi pasipokuwa na hatia yoyote katika siku ya Kristo.
11 Na pia ili mjazwe na tunda la haki lipatikanalo katika Yesu Kristo, kwa utukufu na sifa ya Mungu.
12 Sasa ndugu zangu, nataka mjue kuwa, mambo yaliyotokea kwangu yameifanya injili iendelee sana.
13 Ndiyo maana vifungo vyangu katika Kristo, vimejulikana kwa walinzi wa ikulu yote na kwa kila mtu pia.
14 Na ndugu wengi katika Bwana, kwa sababu ya vifungo vyangu, wameshawishika na kuthubutu kulihubiri Neno pasipo hofu.
15 Baadhi kweli hata humtangaza Kristo kwa fitina na ugomvi, na pia wengine kwa nia njema.
16 Wale wanaomtangaza Kristo kwa upendo wanajua kuwa nimewekwa hapa kwa ajili ya utetezi wa injili.
17 Bali wengine wanamtangaza Kristo kwa ubinafsi na nia mbaya. Hudhani kuwa wanasababisha matatizo kwangu katika minyororo yangu.
18 Kwa hiyo? Sijali, aidha njia ikiwa ni kwa hila au kwa kweli, Kristo anatangazwa, na katika hili ninafurahia! Ndiyo, nitafurahia.
19 kwa kuwa ninajua ya kuwa hili litaleta kufunguliwa kwangu. Jambo hili litatokea kwa sababu ya maombi yenu na kwa msaada wa Roho wa Yesu Kristo.
20 Kulingana na matarajio yangu ya uhakika na kweli ni kwamba, sitaona aibu. Badala yake, kwa ujasiri wote, kama ambavyo siku zote na sasa, natarajia kuwa Kristo atainuliwa katika mwili wangu, ikiwa katika uzima au katika kifo.
21 Kwa maana kwangu mimi, kuishi ni Kristo na kufa ni faida.
22 Lakini, kama kuishi katika mwili huzaa tunda katika kazi yangu, kwa hiyo sijui ni lipi la kuchagua.
23 Maana ninasukumwa sana na mawazo haya mawili. Nina hamu ya kuuacha mwili na kuwa pamoja na Kristo, kitu ambacho ni cha thamani sana sana.
24 Ingawa, kubaki katika mwili huu ni jambo la muhimu sana kwa ajili yenu.
25 Kwa kuwa nina uhakika juu ya hili, ninajua nitabaki na kuendelea kuwa pamoja nanyi nyote, kwa ajili ya maendeleo na furaha ya imani yenu.
26 Na hii italeta furaha yenu kubwa katika Kristo Yesu, kwasababu yangu itaongezeka, kwa sababu ya uwepo wangu tena pamoja nanyi.
27 Mnatakiwa kuishi maisha yenu katika mwenendo mzuri uipasayo injili ya Kristo. fanyeni hivyo ili nikija kuwaona au nisipokuja, nisikie kuwa mmesimama imara katika roho moja. natamani kusikia kuwa mna roho moja, mkiishindania imani ya injili kwa pamoja.
28 na msitishwe na kitu chochote kinachofanywa na maadui zenu. Hii kwao ni ishara ya uharibifu. Bali kwenu ni ishara ya wokovu kutoka kwa Mungu.
29 kwa maana ninyi mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, bali na kuteswa pia katika Yeye.
30 kwa maana mna mgogoro uleule kama mliouona kwangu na mnasikia kwamba ninao hata sasa.