4
1 Wanangu, sikilizeni, fundisho la baba, na zingatieni ili mjue maana ya ufahamu.
2 Mimi ninawapa mafundisho mazuri; msiyaache mafundisho yangu.
3 Mimi nilikuwa mwana kwa baba yangu, mpole na mtoto pekee kwa mama yangu,
4 baba alinifundisha akiniambia, “Moyo wako uzingatie sana maneno yangu; shika amri zangu nawe uishi.
5 Jipatie hekima na ufahamu; usisahau na kuyakataa maneno ya kinywa changu;
6 usiiache hekima nayo itakulinda; ipenda nayo itakuhifadhi salama.
7 Hekima ni kitu cha muhimu sana, hivyo jipatie hekima na tumia namna zote kuweza kupata ufahamu.
8 Tunza hekima nayo itakutukuza; ikumbatie nayo itakuheshimu.
9 Hekima itaweka kilemba cha heshima juu ya kichwa chako; itakupa taji zuri.
10 Mwanangu, sikiliza, na kuzingatia maneno yangu, nawe utapata miaka mingi ya maisha yako.
11 Ninakuelekeza katika njia ya hekima, nimekuongoza katika mapito yaliyonyooka.
12 Unapotembea, hakuna atakayesimama katika njia yako na kama ukikimbia hutajikwaa.
13 Shika mwongozo wala usiuache, utakuongoza, maana ni uzima wako.
14 Usifuate njia ya waovu wala usiende katika njia ya watendao uovu.
15 Jiepushe nayo, usipite katika njia hiyo; geuka na upite njia nyingine.
16 Maana hawawezi kulala mpaka wafanye ubaya na hupotewa na usingizi hadi wasababishe mtu kujikwaa.
17 Maana wao hula mkate wa uovu na hunywa divai ya vurugu.
18 Bali njia ya mwenye kutenda haki ni kama mwanga ung'aao, huangaza zaidi na zaidi hadi mchana inapowasili kwa ukamilifu.
19 Njia ya waovu ni kama giza - hawajui ni kitu gani huwa wanajikwaa juu yake.
20 Mwanangu, zingatia maneno yangu; sikiliza kauli zangu.
21 Usiziache zikaondoka machoni pako; uzitunze katika moyo wako.
22 Maana maneno yangu ni uzima kwa wenye kuyapata na afya katika mwili wao.
23 Ulinde salama moyo wako na uukinge kwa bidii zote; kwa kuwa katika moyo hububujika chemichemi za uzima.
24 Jiepushe na kauli za udanganyifu na ujiepushe na mazungumzo ya ufisadi.
25 Macho yako yatazame mbele kwa unyoofu na kwa uthabiti tazama mbele sawasawa.
26 Usawazishe pito la mguu wako; na njia zako zote zitakuwa salama.
27 Usigeuke upande wa kulia au kushoto; ondoa mguu wako mbali na uovu.