141
Zaburi ya Daudi. Ee Yahwe, ninakulilia wewe; uje upesi kwangu. Unisikilize nikuitapo. Maombi yangu na yawe kama uvumba mbele zako; mikono yangu iliyoinuliwa na iwe kama dhabihu ya jioni. Ee Yahwe, uweke mlinzi kinywani mwangu; mngojezi malangoni pa midomo yangu. Usiruhusu tamaa ya moyo wangu kutamani uovu wowote wala kushiriki katika matendo ya dhambi na watu waishio maovuni. Nisile vyakula vyao vya anasa. Mwenye haki na anipige; nao utakuwa ni wema kwangu. Anirudi; itakuwa kama mafuta kichwani pangu; kichwa changu na kisikatae kupokea. Lakini maombi yangu siku zote yatakuwa dhidi ya matendo yao mauvu. Viongozi wao watatupwa chini toka juu mlimani; watayasikia maneno yangu kuwa ni matamu. Watalazimika kusema, “Kama vile jembe moja livunjapo ardhi, hivyo mifupa yetu imesambaratishwa kinywani pa kuzimu.” Hakika macho yangu yanakutazama wewe, Yahwe, Bwana; katika wewe napata kimbilio; usiiache nafsi yangu. Unilinde dhidi ya mitego waliyoiweka kwa ajili yangu, na matanzi yao watendao maovu. 10 Waovu na waangukie kwenye nyavu zao wenywe pindi mimi nitorokapo.