38
Zaburi ya Daudi, kuirejeza katika kumbukumbu.
1 Yahwe, usinikemee katika hasira yako; usiniadhibu katika ghadhabu yako.
2 Kwa kuwa mishale yako hunichoma, na mkono wako huniangusha chini.
3 Mwili wangu wote unaumwa kwa sababu ya hasira yako; kwa sababu ya dhambi zangu mifupa yangu haina afya.
4 Kwa maana maovu yangu yamenielemea; yamekuwa mzigo mzito kwangu.
5 Vidonda vyangu vimeoza na vinanuka kwa sababu ya upumbavu wa dhambi zangu.
6 Nimepindika na kuwa mnyonge kila siku; ninaenenda katika maombolezo siku zote.
7 Kwa maana ndani yangu, ninaungua; hakuna afya katika mwili wangu.
8 Nimedhohofika na kulemewa sana; ninaugua kwa sababu ya dhiki yangu.
9 Bwana, wewe unaielewa shauku ya ndani kabisa ya moyo wangu, na kuugua kwangu hakujifichika kwako.
10 Moyo wangu unapwita pwita, nguvu zangu zinaniisha, macho yangu yanafifia.
11 Marafiki na ndugu zangu wamenitenga kwa sababu ya hali; majirani zangu hukaa mbali nami.
12 Wale wanaoutafuta uhai wangu hutega mitego kwa ajili yangu. Wao ambao hutafuta kunidhuru huongea maneno ya uharibifu na husema maneno ya uongo siku nzima.
13 Lakini, niko kama mtu kiziwi na sisikii lolote; niko kama mtu bubu ambaye hasemi lolote.
14 Niko kama mtu asiye sikia na mbaye hawezi kujibu.
15 Hakika ninakungoja wewe, Yahwe; wewe utanijibu, Bwana Mungu wangu.
16 Ninasema hivi ili kwamba maadui zangu wasije wakafurahia juu yangu. Ikiwa mguu wangu utateleza, watanifanyia mambo mabaya.
17 Kwa kuwa niko karibu mashakani, na niko katika maumivu ya mara kwa mara.
18 Ninatubu makosa yangu; ninahuzunika kwa dhambi zangu.
19 Lakini maadui zangu ni wengi; wale wanichukiao ni wengi.
20 Wao wananilipa mabaya kwa mema; wanavurumiza shutuma kwangu ingawa nimefuata lililo jema.
21 Usinitelekeze, Yahwe, Mungu wangu, usikae mbali nami.
22 Njoo haraka unisaidie, Bwana, wokovu wangu.