61
Kwa kiongozi wa muziki; kwenye chombo cha nyuzi. Zaburi ya Daudi. Sikia kulia kwangu, shughulikia maombi yangu. Kutokea mwisho wa nchi nitakuita wewe wakati moyo wangu umeelemewa; uniongoze kwenye mwamba ulio juu kuliko mimi. Maana wewe umekuwa kimbilio langu la usalama, nguzo imara dhidi ya adui. Uniache niishi hemani mwako milele! Nipate kimbilio salama chini ya makazi ya mbawa zako. Selah Kwa kuwa wewe, Mungu, umesikia viapo vyangu, wewe umenipa mimi urithi wa wale wanao liheshimu jina lako. Wewe utaongeza maisha ya mfalme; miaka yake itakuwa kama vizazi vingi. Yeye atabakia mbele ya Mungu milele. Nitaliimbia sifa jina lako milele ili kwamba niweze kufanya viapo vyangu kila siku.