8
Kwa kiongozi wa muziki; weka kwenye mtindo wa gittith. Zaburi ya Daudi. Yahweh Bwana wetu, ni jinsi gani jina lako ni tukufu katika dunia yote, wewe ufunuaye utukufu wako juu mbinguni. Kutoka katika midomo ya watoto na vichanga umeumba sifa kwa sababu ya utukufu wako, ili kuwanyamazisha maadui wote na walipa kisasi wote. Ninapozitazama mbingu, ambazo vidole vyako vimeumba, mwezi na nyota, ambazo umeziweka kila mmoja katika nafasi yake, Binadamu ni nani hata umtazame, na watu hata uwajali wao? Umewaumba chini kidogo kuliko viumbe vya mbinguni na umewazunguka na utukufu na heshima. Umemfanya binadamu kutawala kazi ya mikono yako; umeviweka vitu vyote chini ya miguu yake: kondoo na ng'ombe wote, na hata wanyama wa porini, ndege wa angani, na samaki wa baharini, na vyote vipitavyo katika mikondo ya bahari. Yahweh Bwana wetu, ni jinsi gani jina lako ni tukufu katika dunia yote!