82
Zaburi ya Asafu. Mungu amesimama katika kusanyiko la mbinguni; katikati ya miungu anahukumu. Hata lini mtahukumu bila haki na kuonesha upendeleo kwa waovu? Selah Wateteeni maskini na yatima; dumisheni haki kwa aliyetaabishwa na fukara. Muokoeni maskini na muhitaji; watoeni mkononi mwa waovu. Hawajui wala hawaelewi; hutembea gizani; misingi yote ya nchi imebomoka. Mimi nilisema, “Ninyi ni miungu, na ninyi nyote wana wa Mungu aliye Juu. Hata hivyo mtakufa kama wanadamu na mtaanguka kama mmoja wa wakuu.” Uinuke, Ee Mungu, uihukumu nchi, maana unaurithi katika mataifa yote.