13
Kila nafsi na iwe na utii kwa mamlaka ya juu, kwa kuwa hakuna mamlaka isipokuwa imetoka kwa Mungu. Na mamlaka zilizopo zimewekwa na Mungu. Kwa hiyo ambaye anapinga mamlaka hiyo hupinga amri ya Mungu; na wale waipingao watapokea hukumu juu yao wenyewe. Kwa kuwa watawala si tishio kwa watendao mema, bali kwa watendao maovu. Je unatamani kutoogopa mamlaka? Fanya yaliyo mema, na utasifiwa nayo. Kwa kuwa ni mtumishi wa Mungu kwako kwa ajili ya mema. Bali kama utatenda yaliyo maovu, ogopa; kwa kuwa habebi upanga bila sababu. Kwa kuwa ni mtumishi wa Mungu, mlipa kisasi kwa ghadhabu juu ya yule afanyaye uovu. Kwa hiyo inakupasa utii, si tu kwa sababu ya gadhabu, bali pia kwa sababu ya dhamiri. Kwa ajili hii pia unalipa kodi. Kwa kuwa wenye mamlaka ni watumishi wa Mungu, ambao wanaendelea kufanya jambo hili. Mlipeni kila mmoja ambacho wanawadai: kodi kwa astahiliye kodi; ushuru kwa astahiliye ushuru; hofu kwa astahiliye hofu; heshima kwa astahiliye heshima. Msidaiwe na mtu kitu chochote, isipokuwa kupendana ninyi kwa ninyi. Kwa kuwa yeye ampendaye jirani yake ametimiliza sheria. Kwa kuwa, “Hautazini, hautaua, hautaiba, hautatamani,” na kama kuna amri nyingine pia, imejumlishwa katika sentensi hii: “Utampenda jirani yako kama wewe mwenyewe.” 10 Upendo hamdhuru jirani wa mtu. Kwa hiyo, upendo ni ukamilifu wa sheria. 11 Kwa sababu ya hili, mnajua wakati, kwamba tayari ni wakati wa kutoka katika usingizi. Kwa kuwa wokovu wetu umekaribia zaidi ya wakati ule tulio amini kwanza. 12 Usiku umeendelea, na mchana umekaribia. Na tuweke pembeni matendo ya giza, na tuvae silaha za nuru. 13 Na tuenende sawa sawa, kama katika nuru, si kwa sherehe za uovu au ulevi. Na tusienende katika zinaa au tamaa isiyoweza kudhibitiwa, na si katika fitina au wivu. 14 Bali tumvae Bwana Yesu Kristo, na tusiweke nafasi kwa ajili ya mwili, kwa tamaa zake.