8
Kwa hiyo basi hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu. Kwa kuwa kanuni ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imenifanya mimi kuwa huru mbali na kanuni ya dhambi na mauti. Kwa maana kile ambacho sheria ilishindwa kufanya kwa sababu ilikuwa dhaifu katika mwili, Mungu alifanya. Alimtuma Mwana wake wa pekee kwa mfano wa mwili wa dhambi awe sadaka ya dhambi, na akaihukumu dhambi katika mwili. Alifanya hivi ili maagizo ya sheria yatimilizwe ndani yetu, sisi tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali kwa kufuata mambo ya Roho. Wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili, lakini wale waifuatao Roho huyafikiri mambo ya Roho. Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti, bali nia ya Roho ni uzima na amani. Hii ni kwa sababu ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii. Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu. Hata hivyo, hampo katika mwili bali katika Roho, kama ni kweli kwamba Roho wa Mungu huishi ndani yenu. Lakini kama mtu hana Roho wa Kristo, yeye si wake. 10 Kama Kristo yumo ndani yenu, mwili umekufa kwa mambo ya dhambi, bali roho ni hai kwa mambo ya haki. 11 Ikiwa Roho wa yule aliyemfufua Yesu kutoka wafu huishi ndani yenu, yeye yule aliyemfufua Kristo kutoka katika wafu ataipa pia miili yenu ya mauti uhai kwa njia ya Roho wake, aishie ndani yenu. 12 Hivyo basi, ndugu zangu, sisi tu wadeni, lakini si kwa mwili kwamba tuishi kwa jinsi ya mwili. 13 Maana ikiwa mnaishi kwa jinsi ya mwili, mpo karibu kufa, lakini ikiwa kwa Roho mnayafisha matendo ya mwili, nanyi mtaishi. 14 Maana kama ambavyo wengi wanaongozwa na Roho wa Mungu, hawa ni wana wa Mungu. 15 Kwa kuwa hamkupokea roho wa utumwa tena hata muogope. Badala yake, mlipokea roho ya kufanywa kuwa wana, ambayo kwayo tunalia, “Abba, Baba!” 16 Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu ya kuwa tu watoto wa Mungu. 17 Ikiwa tu watoto, basi tu warithi pia, warithi wa Mungu. Na sisi tu warithi pamoja na Kristo, ikiwa kwa kweli tunateseka na yeye ili tupate kutukuzwa pamoja naye. 18 Kwa kuwa nayahesabu mateso ya wakati huu kuwa si kitu nikilinganisha na utukufu utakaofunuliwa kwetu. 19 Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu. 20 Kwa maana uumbaji pia ulitiishwa chini ya ubatili, si kwa hiari yake, ila kwa sababu yake yeye aliyevitiisha. Ni katika tumaini 21 kwamba uumbaji wenyewe nao utawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu, na kuingizwa katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu. 22 Kwa maana twajua ya kuwa uumbaji nao pia unaugua na kuteseka kwa uchungu pamoja hata sasa. 23 Si hivyo tu, ila na sisi wenyewe tulio na malimbuko ya Roho - sisi pia tunaugua katika nafsi zetu, tukisubiri kufanywa wana, yaani ukombozi wa miili yetu. 24 Kwa maana ni kwa taraja hili tuliokolewa. Lakini kitu kilichotarajiwa kikionekana hakuna taraja tena, kwa maana ni nani anayekitarajia kile akionacho? 25 Bali tukikitarajia kitu tusichokiona, twakingojea kwa saburi. 26 Kwa jinsi iyo hiyo, Roho naye hutusaidia katika udhaifu wetu. Kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. 27 Na yeye aichunguzaye mioyo huijua akili ya Roho, kwa sababu huomba kwa niaba yao walioamini kulingana na mapenzi ya Mungu. 28 Nasi twajua ya kuwa kwa wote wampendao Mungu, yeye hufanya mambo yote pamoja kwa wema, kwa wale wote walioitwa kwa kusudi lake. 29 Kwa sababu wale wote aliowajua tangu asili, pia aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miogoni mwa ndugu wengi. 30 Na wale aliowachagua tangu asili, hao aliwaita pia. Na wale aliowaita, hao aliwahesabia haki. Na wale aliowahesabia haki, hao pia akawatukuza. 31 Tuseme nini basi juu ya mambo haya? Mungu akiwa upande wetu, ni nani aliye juu yetu? 32 Yeye asiyemwachilia mwana wake mwenyewe bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye? 33 Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. 34 Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa kwa ajili yetu, na zaidi ya hayo, yeye pia alifufuliwa. Naye anatawala pamoja na Mungu mahali pa heshima, na tena ndiye anayetuombea sisi. 35 Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Dhiki, au shida, au mateso, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? 36 Kama ilivyoandikwa, “Kwa faida yako tunauawa mchana kutwa. Tulihesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa.” 37 Katika mambo haya yote sisi tu zaidi ya washindi katika yeye aliyetupenda. 38 Kwa maana nimekwisha kushawishika kwamba wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala mamlaka, wala vitu vilivyopo, wala vitu vijavyo, wala nguvu, 39 wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote, hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu, ambaye ni Kristo Yesu Bwana wetu.