12
1 Samweli aksema na Israeli wote, “Nimesikia kila kitu mlichoniambia, na nimemweka mfalme juu yenu.
2 Basi, yupo hapa mfalme aliyeko mbele yenu, mimi nimezeeka nakujaa mvi; na watoto wangu wako pamoja nanyi. Nimekuwa kiongozi wenu tangu ujana wangu hadi leo.
3 Mimi niko hapa, Nishuhudieni mbele za BWANA na mbele za mtiwa mafuta wake. Nimechukua ng'ombe wa nani? Nimechukua punda wa nani? Ni nani nimemdhulumu? Nimemwonea nani? Nimepokea rushwa kutoka mikono ya nani inipofushe macho yangu? Nishuhudieni, nami nitawarudishia
4 Nao wakasema, Haujatudanganya, kutuonea, au kuiba chochote kutoka mkono wa mtu yeyote.”
5 Akawaambia, “BWANA ni shahidi juu yenu, na masihi wake leo ni shahidi, kwamba hamkuona kitu mkononi mwangu.” Na wao wakajibu, “BWANAni shahidi.”
6 Samweli akawaambia watu, “BWANA ndiye aliyemteua Musa na Haruni, na ndiye aliyewatoa baba zenu kutoka nchi ya Misri.
7 Basi sasa, jihudhurisheni, ili niweze kutoa utetezi juu yenu kwa BWANA kuhusu matendo yote ya haki ya BWANA, ambayo aliwafanyia ninyi na baba zenu.
8 Yakobo alipokuwa amefika Misri, na babu zenu walimlilia BWANA. BWANA alimtuma Musa na Haruni, waliowaongoza babu zenu kutoka Misri na wakaja kukaa sehemu hii.
9 Lakini walimsahau BWANA Mungu wao; akawauza katika mkono wa Sisera, jemedari wa majeshi ya Hazori, katika mkono wa Wafilisti, na katika mkono wa mfalme wa Moabu; hawa wote walipigana na babu zenu.
10 Wakamlilia BWANA mkasema, 'Tumefanya dhambi, kwa sababu tumemwacha BWANA na tumewatumikia Mabaali na Mashtorethi. Lakini sasa tuokoe kutoka mikono ya maadui zetu, na tutakutumikia.'
11 Hivyo BWANA akawatuma Yerubu Baali, Bedani, Yefta na Samweli, na akawapa ushindi dhidi ya maadui zenu wote waliowazunguka, na kwamba mliishi kwa amani.
12 Mlipoona kwamba Nahashi mfalme wa watu wa Amoni amekuja dhidi yenu, mkaniambia, 'Hapana! Badala yake, mfalme awepo atawale juu yetu'- ingawa BWANA, Mungu wenu, alikuwa mfalme wenu.
13 Sasa yupo hapa mfalme ambaye mmemchagua, mliyemuomba na ambaye BWANA amemteua awe mfalme juu yenu.
14 Ikiwa mnamhofu BWANA, mtumikieni, muitii sauti yake, msikaidi amri ya BWANA, basi wote wawili ninyi na mfalme anayewatawala mtakuwa wafuasi wa BWANA Mungu wenu.
15 Kama hamtaitii sauti ya BWANA, mkaasi amri za BWANA, ndipo mkono wa BWANA utakuwa juu yenu, kama ulivyokuwa juu ya babu zenu.
16 Hata sasa muwepo kabisa na muone jambo kubwa ambalo BWANA atalifanya mbele ya macho yenu.
17 Je, leo si mavuno ya ngano? Nitamwomba BWANA, naye ataleta ngurumo na mvua. Ndipo mtajua na kuona kwamba uovu wenu ni mwingi, mlioufanya machoni pa BWANA, kujiombea mfalme wenu ninyi wenyewe.”
18 Hivyo Samweli akamwomba BWANA; na siku iyo hiyo BWANA akatuma ngurumo na mvua. Ndipo watu wote wakamwogopa sana BWANA pamoja na Samweli.
19 Kisha watu wote wakamwambia Samweli, “Waombee watumishi wako kwa BWANA Mungu wako, ili tusife. Kwa maana tumeongeza uovu huu juu ya dhambi zetu tulipojiombea mfalme sisi wenyewe.”
20 Samweli akawajibu, “Msiogope. Mmefanya uovu wote huu, lakini msigeukie mbali na BWANA, bali mtumikieni BWANA kwa moyo wenu wote.
21 Wala msigeuke na kufuata mambo matupu yasiyo na faida au kuwaokoa, kwa sababu ni ubatili.
22 Kwa ajili ya jina lake kuu, BWANA hatawakataa watu wake, kwa sababu imempendeza BWANA kuwafanya ninyi kuwa watu kwa ajili yake.
23 Kwangu mimi, iwe mbali nami kumtenda BWANA dhambi kwa kuacha kuwaombea ninyi. Badala yake, nitawafundisha njia iliyo njema na sahihi.
24 Mcheni BWANA tu na mtumikieni yeye katika kweli kwa moyo wenu wote. Tafakarini mambo makuu aliyowatendeeni.
25 Lakini kama mtadumu kufanya uovu, ninyi wote na mfalme wenu mtaangamizwa.”