10
1 Ikawa baadaye mfalme wa watu wa Amoni akafa, na Hanuni mwanaye akawa mfalme mahali pake.
2 Daudi akasema, “Nitaonesha fadhiri Hanuni mwana wa Nahashi, kwa kuwa baba yake alinifadhiri.” Hivyo Daudi akatuma watumishi wake kumfariji Hanuni kwa habari ya baba yake. Watumishi wake wakaingia katika nchi ya watu wa Amoni.
3 Lakini viongozi wa watu wa Amoni wakamwambia Hanuni bwana wao, “Je unathani kwa hakika Daudi anamweshimu baba yako hata ametuma watu kukutia moyo? Daudi hajawatuma watumishi wake kwako ili kuuangalia mji, kuupeleleza, ili kuupindua?
4 Hivyo Hanuni akawachukuwa watumishi wa Daudi, akawanyoa nusu ya ndevu zao, akachana mavazi yao hadi kwenye matako, naye akawaacha waende zao.
5 Daudi alipoelezwa kuhusu hili, akatuma watu kwenda kuwalaki, kwa kuwa walikuwa wamefedheheshwa sana. Mfalme akawambia, “Kaeni Yeriko mpaka ndevu zenu zitakapoota, ndipo mrudi.”
6 Watu wa Amoni walipoona kwamba wamenuka kwa Daudi, wakatuma wajumbe na kuwaajiri Washami wa Bethi Rehobu na Soba, askari elfu ishirini waendao kwa mguu, na mfalme wa Maaka pamoja na watu elfu, na watu wa Tobu elfu kumi na mbili.
7 Daudi aliposikia, akamtuma Yoabu na jeshi lote la askari.
8 Waamoni wakatoka na wakafanya mistari ya vita katika maingilio ya lango la mji wao, wakati Washami wa Soba na wale wa Rehobu, na watu wa Tobu na Maaka, wakasimama peke yao uwandani.
9 Yoabu alipoona mistari ya vita ikimkabili pote mbele na nyuma, alichagua baadhi ya waisraeli wajuao kupigana vizuri na akawapanga dhidi ya Washami.
10 Na sehemu iliyosalia ya jeshi, akawaweka chini ya Abishai nduguye, naye akawaweka katika mistari ya vita dhidi ya jeshi la Amoni.
11 Yoabu akasema, “ikiwa Washami watakuwa na nguvu zaidi juu yangu, kisha wewe, Abishai, lazima uniokoe. Lakini ikiwa jeshi la Amoni litakuwa na nguvu zaidi juu yako, nitakuja kukuokoa.
12 Iweni na nguvu, nasi tujioneshe kuwa wenye nguvu kwa ajili ya watu wetu na miji ya Mungu wetu, kwa maana Yahwe atatenda yapendezayo kwa ajili ya kusudi lake.
13 Hivyo Yoabu na askari wa jeshi lake wakasonga mbele katika vita dhidi ya Washami, waliolazimika kukimbia mbele ya jeshi la Israeli.
14 Jeshi la Amoni lilipoona kwamba Washami wamekimbia, nao pia wakakimbia kutoka kwa Abishai wakarudi ndani ya mji. Ndipo Yoabu akarudi kutoka kwa watu wa Amoni na akarejea Yerusalemu.
15 Washami walipoona kwamba wameshindwa na Israeli, walijikusanya pamoja tena.
16 Kisha Hadareza akatuma kuleta vikosi vya Washami ng'ambo ya Mto Frati. Wakaja Helamu pamoja na Shobaki, mkuu wa jeshi la Hadareza juu yao.
17 Daudi alipoambiwa, aliwakusanya Israeli wote pamoja, akavuka Yordani, na akafika Helamu. Washami wakajipanga katika mistari ya vita dhidi ya Daudi na wakapigana naye.
18 Washami wakakimbia mbele ya Israeli. Daudi akaua askari mia saba wa magari na askari wa farasi elfu arobaini. Shobaki mkuu wa jeshi lao alijeruhiwa na akafa huko.
19 Wafalme wote waliokuwa watumishi wa Hadareza walipoona kuwa wameshindwa na Israeli, walifanya amani na Israeli na wakawa watumishi wao. Hivyo washami wakaogopa kuwasaidia watu wa Amoni tena.