12
1 Kisha Yahwe akamtuma Nathani kwa Daudi. Akaja kwake na kusema, “Kulikuwa na watu wawili katika mji. Mmoja alikuwa tajiri na mwingine alikuwa masikini.
2 Yule tajiri alikuwa na kundi la ng'ombe na kondoo wengi sana,
3 lakini maskini hakuwa na chochote isipokuwa mwanakondoo, aliyekuwa amemnunua na kumlisha na kumlea. Akakua pamoja naye na pamoja na watoto wake. Yule mwanakondoo hata alikula naye na kunywa kutoka katika kikombe chake, naye akalala katika mikono yake na alikuwa kama binti kwake.
4 Siku moja tajiri akapata mgeni, lakini yeye hakuwa tiyari kuchukua mnyama kutoka katika kundi lake la ng'ombe au kundi la kondoo ili kumwandalia chakula. Badala yake alichukua mwanakondoo wa masikini na akampika kwa ajili ya mgeni wake.
5 Hasira ya Daudi ikawaka dhidi ya tajiri yule, naye akamwambia Nathani kwa hasira, “Kama Yahwe aishivyo, mtu aliyelitenda jambo hili anastahili kufa.
6 Ni lazima alipe mwanakondoo mara nne zaidi kwa ajili ya kile alichokifanya, na kwa sababu hakuwa na huruma kwa mtu maskini.
7 Ndipo Nathani akamwambia Daudi, “Wewe ndiye yule mtu! Yahweh, Mungu wa Israeli, asema, 'Nilikutia mafuta uwe mfalme juu ya Israeli, na nilikuokoa kutoka katika mkono wa Sauli.
8 Nikakupa nyumba ya bwana wako, na wake zake mikononi mwako. Nilikupa pia nyumba ya Israeli na Yuda. Na ikiwa hayo yalikuwa kidogo zaidi kwako, ningeweza kukuongezea mengine zaidi.
9 Hivyo basi kwa nini umedharau maagizo ya Yahwe, hata ukafanya yaliyo maovu mbele zake? Umeua Uria Mhiti kwa upanga na umechukua mkewe kuwa mke wako. Uliua kwa upanga wa jeshi la Amoni.
10 Hivyo basi upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa kuwa umenidharau na umemchukua mke wa Uria mhiti kuwa mke wako.'
11 Yahwe asema, 'Tazama, nitaleta maafa dhidi yako kutoka katika nyumba yako mwenyewe. Nitachukua wake zako, mbele ya macho yako na kumpa jirani yako, naye atalala na wake zako wakati wa mchana.
12 Kwa maana wewe ulitenda dhambi hii sirini, lakini mimi nitatenda jambo hili wakati wa mchana mbele za Israeli wote.
13 Ndipo Daudi alipomwambia Nathani, “Nimemtenda dhambi Yahwe.” Nathani akamjibu Daudi, “Yahwe naye ameiachilia dhambi yako. Hautakufa.
14 Lakini, kwa kuwa kwa tendo hili umemdharau Yahwe, mtoto aliyezaliwa kwako hakika atakufa.”
15 Kisha Nathani akaondoka na kwenda kwake. Yahwe akampiga mtoto ambaye mke wa Uria alimzaa kwa Daudi, naye akaugua sana.
16 Kisha Daudi akamwomba Mungu kwa ajili ya kijana. Daudi akafunga naye akaingia ndani na kulala usiku wote juu ya sakafu.
17 Wazee wa nyumba yake wakainuka na kusimama kando yake, ili wamwinue kutoka sakafuni. Lakini hakuinuka, na hakula pamoja nao.
18 Ikawa siku ya saba mtoto akafa. Watumishi wa Daudi wakaogopa kumwambia kwamba mtoto amekufa, kwa maana walisema, “Tazama, wakati mtoto alipokuwa hai tuliongea naye, lakini hakuisikiliza sauti yetu. Atakuwaje ikiwa tutamwambia kwamba kijana amekufa?!”
19 Daudi alipoona kwamba watumishi wake walikuwa wakinong'onezana, Akatambua kwamba mtoto amekufa. Akawauliza, “Je mtoto amekufa?” Wakajibu, “Amekufa.”
20 Kisha Daudi akainuka kutoka sakafuni naye akaoga, akajipaka mafuta, na kubadili mavazi yake. Akaenda katika hema la kukutania na akaabudu pale, kisha akarudu katika kasri lake. Akataka chakula kiletwe, wakamwandalia, naye akala.
21 Ndipo watumishi wake walipomwambia, “Kwa nini umefanya jambo hili? Ulifunga na kulia kwa ajili ya mtoto wakati alipokuwa hai, lakini mtoto alipokufa, ukainuka na kula.”
22 Daudi akajibu, “Wakati mtoto alipokuwa hai nilifunga na kulia. Nilisema, Ni nani ajuaye kwamba Yahwe angeweza kunihurumia mtoto akaishi au sivyo?
23 Lakini sasa amekufa, hivyo nifungie nini? Je naweza kumrudisha tena? Nitakwenda kwake, lakini yeye hawezi kunirudia.”
24 Daudi akamfariji Bethsheba mkewe, akaingia kwake, na akalala naye. Baadaye akazaa mtoto wa kiume, naye akaitwa Selemani. Yahwe akampenda
25 naye akatuma neno kupitia nabii Nathani kumwita Yedidia, kwa sababu Yahwe alimpenda.
26 Basi Yoabu akapigana na Raba, mji wa kifalme wa watu wa Amoni, naye akaiteka ngome yake.
27 Hivyo Yoabu akatuma wajumbe kwa Daudi na kusema, “Nimepigana na Raba, nami nimeshikilia sehemu inayosambaza maji ya mji.
28 Kwa hiyo sasa likusanye jeshi lililosalia uhuzingire mji na kuuteka, kwa maana ikiwa nitauteka, utaitwa kwa jina langu.”
29 Hivyo Daudi akalikusanya jeshi lote na kwenda Raba; akapigana nao na kuuteka.
30 Daudi akachukua taji ya dhahabu kutoka katika kichwa cha mfalme wao iliyokuwa na uzito wa talanta, na ilikuwa na jiwe la thamani ndani yake. Taji ikawekwa juu ya kichwa cha Daudi. Kisha akachukua nyara za mji kwa wingi.
31 Akawatoa watu waliokuwa mjini naye akawalazimisha kufanya kazi kwa misumeno, sululu na shoka; lakini pia akawalazimisha kutengeneza matofali. Daudi akailazimisha miji yote ya watu wa Amoni kufanya kazi hiyo. Kisha Daudi na jeshi lote wakarudi Yerusalemu