2 Timotheo
1
1 Paulo mtume wa Yesu Kristo kwa mapenzi ya Mungu, sawasawa na ahadi ya uzima ulio ndani ya Kristo Yesu,
2 kwa Timotheo mwana mpendwa: Neema, rehema na amani toka kwa Mungu Baba na Kristo Yesu Bwana wetu.
3 Ninamshukuru Mungu, ambaye ninamtumikia kwa nia njema kama walivyofanya baba zangu, ninapokumbuka daima katika maombi yangu. Usiku na
4 mchana ninatamani kukuona, ili kwamba nijawe na furaha. Ninayakumbuka machozi yako.
5 Nimekuwa nikikumbushwa kuhusu imani yako halisi, ambayo hapo kwanza ilikaa kwa bibi yako Loisi na mama yako Yunisi. Na nina hakika ya kwamba imani hiyo inakaa ndani yako pia.
6 Hii ndiyo sababu nakukumbusha kuchochea karama ya Mungu iliyomo ndani yako kwa njia ya kuwekewa mikono yangu.
7 Kwa kuwa Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na upendo na nidhamu.
8 Kwa hiyo usiuonee haya ushuhuda kuhusu Bwana wetu, wala wangu mimi Paulo mfungwa wake. Bali ushiriki mateso kwa ajili ya injili sawasawa na uweza wa Mungu.
9 Ni Mungu aliyetuokoa na kutuita kwa wito mtakatifu. Hakufanya hivi kulingana na kazi zetu bali kulingana na neema na mpango wake mwenyewe. Alitupatia mambo haya katika Kristo Yesu kabla ya nyakati kuanza.
10 Lakini sasa wokovu wa Mungu umekwishafunuliwa kwa kuja kwa mwokozi wetu Kristo Yesu. Ni Kristo aliyeikomesha mauti na kuleta uzima usiokoma kwa nuru ya injili.
11 Kwa sababu hiyo nilichaguliwa kuwa mhubiri, mtume na mwalimu.
12 Kwa sababu hii nateseka pia, lakini sioni haya kwa kuwa namjua yeye niliyekwisha kumuamini. Nina hakika kuwa yeye anaweza kukitunza kile nilichokikabidhi kwake hata siku ile.
13 Ukumbuke mfano wa ujumbe wa uaminifu uliousikia toka kwangu, pamoja na imani na upendo ulio ndani ya Kristo Yesu.
14 Yatunze Mambo mazuri aliyokukabidhi Mungu kupitia Roho Mtakatifu aishiye ndani yetu.
15 Unajua ya kuwa, wote waishio katika Asia waliniacha. Kwenye kundi hili wamo Figelo na Hemogene.
16 Bwana airehemu nyumba ya Onesiforo kwa kuwa mara nyingi aliniburudisha na hakuionea aibu minyororo yangu.
17 Badala yake, alipokuwa Roma alinitafuta kwa bidii na akanipata.
18 Mungu amjalie kupata rehema kutoka kwake siku ile. Kama alivyonisaidia nilipokuwa Efeso, wewe wajua vyema.