Tito
1
1 Paulo, mtumishi wa Mungu na mtume wa Yesu Kristo, kwa imani ya wateule wa Mungu na maarifa ya kweli iletayo utauwa.
2 Wapo katika tumaini la uzima wa milele ambao Mungu asiyeweza kusema uongo aliuahidi tangu milele.
3 Kwa wakati muafaka, alilifunua neno lake katika ujumbe alionipa mimi kuhubiri. Ilinipasa kufanya hivi kwa amri ya Mungu mwokozi wetu.
4 Kwa Tito, mwana wa kweli katika imani yetu. Neema, huruma na amani kutoka kwa Mungu Baba na Yesu Kristo mwokozi wetu.
5 Kwa sababu hii nalikuacha Krete, kwamba uyatengeneze mambo yote yaliyokuwa hayajakamilika na kuweka wazee wa kanisa kwa kila mji kama nilivyokuagiza.
6 Mzee wa kanisa lazima asiwe na lawama, mme wa mke mmoja, aliye na watoto waaminifu wasioshuhudiwa mabaya au wasio na nidhamu.
7 Ni muhimu kwa mwangalizi, kama msimamizi wa nyumba ya Mungu, asiwe na lawama. Asiwe mtu wa kelele au asiye jizuia. Lazima asiwe mwepesi wa hasira, asiwe mlevi, asiwe mtu wa kusababisha ugomvi, na asiwe mwenye tamaa.
8 Badala yake: awe mtu mkaribishaji, apendaye wema. Lazima awe mtu mwenye akili timamu, mwenye haki, mcha Mungu, anayejitawala mwenyewe.
9 Awezaye kusimamia mafundisho ya kweli yaliyofundishwa, ili aweze kuwatia moyo kwa mafundisho mazuri na awezaye kuwarekebisha wote wanaompinga.
10 Kwa kuwa kuna waasi wengi, hasa wale wa tohara. Maneno yao ni ya upuuzi. Wanadanganya na kuwaongoza watu katika upotovu.
11 Ni lazima kuwazuia watu kama hao. Wanafundisha yale wasiyopaswa kwa faida za aibu na kuharibu familia zote.
12 Mmoja wao, mtu mwenye busara, alisema, “Wakrete wana uongo usio na mwisho, wabaya na wanyama wa hatari, wavivu na walafi.”
13 Haya maelezo ni ya kweli, kwa hiyo uwazuie kwa nguvu ili kwamba waweze kusema kweli katika imani.
14 Wewe usijihusishe na hadithi zisizo za kweli za Kiyahudi au amri za watu, ambao hurudisha nyuma ukweli.
15 Kwa wote walio safi, vitu vyote ni visafi. Lakini kwa wote walio wachafu na wasioamini, hakuna kilicho kisafi. Kwa kuwa mawazo yao na dhamira zao zimechafuliwa.
16 Wanakiri kumjua Mungu, lakini kwa matendo yao wanamkana. Wao ni waovu na wasiotii. Hawakuthibitishwa kwa tendo lolote jema.