13
Katika siku hiyo kijito kitafunguliwa kwa ajili ya nyumba ya Daudi na wenyeji wa Yerusalemu, kwa ajili ya dhambi na uchafu wao. Katika siku hiyo - asema Yahwe wa majeshi - kwamba nitaondoa majina ya sanamu katika nchi ili kwamba yasikumbukwe tena. Nitawaondoa pia katika nchi manabii wa uongo na roho wao mchafu Ikiwa mtu yeyote ataendelea kutoa unabii, baba yake na mama yake waliomzaa watamwambia, 'Hautaishi, kwa kuwa umenena uongo kwa jina la Yahwe! Ndipo baba na mama waliomzaa watakapomchoma wakati akitabiri. Katika siku hiyo kila nabii ataonea aibu maono yake aelekeapo kutoa unabii. Manabii hawa hawatavaa tena vazi la singa, ili kuwadanganya watu. Kwa maana kila mmoja atasema, 'Mimi siyo nabii! mimi ni mkulima, kwa maana ardhi ndiyo kazi yangu tangu ujana wangu! Lakini mtu mwingine atamwambia, 'Majeraha haya kati ya mikono yako ni ya nini?' naye atajibu, nilijeruhiwa na waliokuwa katika nyumba ya rafiki zangu.” Upanga! inuka mwenyewe dhidi ya mchungaji wangu, mtu asimamaye karibu nami - hivi ndivyo asemavyo Yahwe wa majeshi. Mpige mchungaji, na kondoo watatawanyika! Kwa maana nitageuza mkono wangu dhidi ya wadogo. Kisha itakuwa kwamba katika nchi yote - hivi ndivyo asemavyo Yahwe - kwamba theluthi mbili yake itaondolewa! Watu hao wataangamia; theluthi moja tu ndiyo itakayosalia. Nitaipitisha hiyo ya tatu motoni na kuwasafisha kama fedha isafishwavyo; nitawajaribu kama dhahabu ijaribiwavyo. Wataliitia jina langu nami nitawajibu na kusema, 'Hawa ni watu wangu!' nao watasema, Yahwe ndiye Mungu wangu!”