8
1 Neno la Yahwe wa majeshi likanijia kusema,
2 “Yahwe wa majeshi asema hivi: Nina huzuni kwa ajili ya Sayuni kwa wivu mkuu na ninamaumivu kwa hasira nyingi!
3 Yahwe wa majeshi asema hivi: Nitairudia Sayuni nami nitakaa kati ya Yerusalemu, kwa kuwa Yerusalemu itaitwa mji wa kweli na mlima wa Yahwe wa majeshi utaitwa Mlima Mtakatifu!
4 Yahwe wa majeshi asema hivi: Kwa mara nyingine tena kutakuwa na vikongwe katika mitaa ya Yerusalemu, na kila mtu ataitaji mkongojo mkononi mwake kwa vile alivyo mzee.
5 Pia mitaa ya mji itajazwa na vijana wa kiume na kike wachezao.
6 Yahwe wa majeshi asema hivi: ikiwa jambo laonekana haliwezekani katika macho ya masalia ya watu hawa katika siku hizo, je haliwezekani pia machoni pangu? - asema Yahwe.
7 Yahwe wa majeshi asema hivi: Tazama, nipo tayari kuwaokoa watu wangu kutoka nchi ya mawio na ya machweo ya jua!
8 Kwa maana nitawarudisha tena, nao wataishi ndani ya Yerusalemu, hivyo watakuwa watu wangu tena, nami nitakuwa Mungu wao katika kweli na utakatifu!
9 Yahwe wa majeshi asema hivi: Ninyi mnaoendelea kusikia maneno yaleyale yaliyotoka katika vinywa vya manabii msingi wa nyumba yangu ulipowekwa - hii nyumba yangu, Yahwe wa majeshi: Itieni nguvu mikono yenu ili hekalu lijengwe.
10 Kwani kabla ya siku hizo hakuna mazao yaliyokusanywa na yeyote ndani yake, hakukuwa na faida siyo kwa mtu hata mnyama, na hakukuwa na amani kutoka kwa adui kwa kila aliyekwenda au kuja. Nilimfanya kila mtu kuwa kinyume cha mwenzake.
11 Lakini sasa haitakuwa kama mwanzo, nitakuwa pamoja na masalia ya watu hawa - asema Yahwe wa majeshi.
12 Kwani mbegu za amani zitapandwa; mzabibu unaokua utatoa matunda yake na nchi itatoa mazao yake; anga zitatoa umande, kwa maana nitawapa masalia ya watu hawa kumilki haya yote.
13 Ulikuwa mfano wa laana kwa mataifa mengine, enyi nyumba ya Yuda na nyumba ya Israeli. Hivyo nitawaokoa nanyi mtakuwa baraka. Msiogope; haya mikono yenu itiwe nguvu!
14 Kwa maana Yahwe wa majeshi asema hivi: Kama nilivyopanga kuwatenda mabaya babu zenu walipochokoza hasira yangu - asema Yahwe wa majeshi - na wala sikujuta,
15 ndivyo nitakavyoazimia kuutenda mema tena Yerusalemu na nyumba ya Yuda katika siku hizi! Msiogope!
16 Haya ndiyo mambo mnayopaswa kufanya: Kasemeni kweli, kila mtu na jirani yake. Hukumuni kwa haki, usawa na amani katika malango yenu.
17 Na asiwepo miongoni mwenu anayeazimu uovu moyoni mwake dhidi ya jirani yake, wala kuvutwa na viapo vya uongo; kwani haya yote ndiyo mambo ninayoyachukia! - asema Yahwe.”
18 Kisha neno la Yahwe wa majeshi likanijia kusema,
19 “Yahwe wa majeshi asema hivi: Mifungo ya mwezi wa nne, mwezi wa tano, mwezi wa saba na mwezi wa kumi itakuwa nyakati za furaha ya kila aina, kwa nyumba ya Yuda! Kwa hiyo pendeni kweli na amani!
20 Yahwe wa majeshi asema hivi: Watu watakuja tena, hata wanaoishi miji mingine.
21 Watu wa mji mmoja watakwenda mji mwingine na kusema, “Haya twendeni haraka mbele ya Yahwe tukaombe na kumtafuta Yahwe wa majeshi! Sisi wenyewe tunakwenda pia.
22 Watu wengi na mataifa yenye nguvu yatakuja kumtafuta Yahwe wa majeshi huko Yerusalemu na kuomba upendeleo kwa Yahwe!
23 Yahwe wa majeshi asema hivi: Katika siku hizo watu kumi kutoka katika kila lugha na taifa watashika upindo wa kanzu zenu na kusema, “Haya sisi nasi tutakwenda pamoja nanyi, kwani tumesikia kwamba Mungu yu pamoja nayi!”