11
Tawi Kutoka Kwa Yese
Chipukizi litatokea kutoka shina la Yese,
kutoka mizizi yake Tawi litazaa tunda.
Roho wa Bwana atakaa juu yake,
Roho wa hekima na wa ufahamu,
Roho wa shauri na wa uweza,
Roho wa maarifa na wa kumcha Bwana
naye atafurahia kumcha Bwana.
 
Hatahukumu kwa yale ayaonayo kwa macho yake,
wala kuamua kwa yale ayasikiayo kwa masikio yake,
bali kwa uadilifu atahukumu wahitaji,
kwa haki ataamua wanyenyekevu wa dunia.
Ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake,
kwa pumzi ya midomo yake atawaua waovu.
Haki itakuwa mkanda wake
na uaminifu utakuwa mshipi kiunoni mwake.
 
Mbwa mwitu ataishi pamoja na mwana-kondoo,
naye chui atalala pamoja na mbuzi,
ndama, mwana simba na ngʼombe wa mwaka mmoja watakaa pamoja,
naye mtoto mdogo atawaongoza.
Ngʼombe na dubu watalisha pamoja,
watoto wao watalala pamoja,
na simba atakula majani makavu kama maksai.
Mtoto mchanga atacheza karibu na shimo la nyoka,
naye mtoto mdogo ataweka mkono wake
kwenye kiota cha fira.
Hawatadhuru wala kuharibu
juu ya mlima wangu mtakatifu wote,
kwa kuwa dunia itajawa na kumjua Bwana
kama maji yajazavyo bahari.
10 Katika siku hiyo, Shina la Yese atasimama kama bendera kwa ajili ya mataifa. Mataifa yatakusanyika kwake, na mahali pake pa kupumzikia patakuwa utukufu. 11 Katika siku hiyo Bwana atanyoosha mkono wake mara ya pili kurudisha mabaki ya watu wake waliosalia kutoka Ashuru, Misri, Pathrosi,* Kushi, Elamu, Babeli, Hamathi na kutoka visiwa vya baharini.
12 Atainua bendera kwa mataifa
na kuwakusanya Waisraeli walioko uhamishoni;
atawakusanya watu wa Yuda waliotawanyika
kutoka pembe nne za dunia.
13 Wivu wa Efraimu utatoweka,
na adui wa Yuda watakatiliwa mbali;
Efraimu hatamwonea Yuda wivu,
wala Yuda hatakuwa na uadui na Efraimu.
14 Watawashukia katika miteremko ya Wafilisti
hadi upande wa magharibi,
kwa pamoja watawateka watu nyara
hadi upande wa mashariki.
Watawapiga Edomu na Moabu,
na Waamoni watatawaliwa nao.
15 Bwana atakausha
ghuba ya bahari ya Misri;
kwa upepo mkavu ataupeleka mkono wake
juu ya Mto Frati.
Ataugawanya katika vijito saba
ili watu waweze kuuvuka wakiwa wamevaa viatu.
16 Itakuwepo njia kuu kwa mabaki ya watu wake
wale waliosalia kutoka Ashuru,
kama ilivyokuwa kwa Israeli
walipopanda kutoka Misri.
* 11:11 Pathrosi ina maana Misri ya Juu.