38
Kuugua Kwa Mfalme Hezekia
(2 Wafalme 20:1-11; 2 Nyakati 32:24-26)
Katika siku hizo Hezekia akaugua, naye akawa karibu kufa. Nabii Isaya mwana wa Amozi akaenda kwake na kumwambia, “Hili ndilo asemalo Bwana: Tengeneza mambo ya nyumba yako, kwa sababu utakufa, hutapona.”
Hezekia akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana: “Ee Bwana, kumbuka jinsi nilivyoenenda mbele zako kwa uaminifu na kujitoa kwa moyo wangu wote, na kufanya yaliyo mema machoni pako.” Naye Hezekia akalia kwa uchungu.
Ndipo neno la Bwana likamjia Isaya, kusema: “Nenda ukamwambie Hezekia, ‘Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa baba yako Daudi: Nimeyasikia maombi yako na nimeona machozi yako. Nitakuongezea miaka kumi na mitano katika maisha yako. Nami nitakuokoa wewe pamoja na mji huu mkononi mwa mfalme wa Ashuru. Nitaulinda mji huu.
“ ‘Hii ndiyo ishara ya Bwana kwako ya kwamba Bwana atafanya kile alichoahidi: Nitafanya kivuli cha jua kwenye ngazi iliyojengwa na Ahazi kirudi nyuma madaraja kumi.’ ” Hivyo jua likarudi nyuma madaraja kumi ambayo lilikuwa limeshuka.
 
Maandiko ya Hezekia mfalme wa Yuda baada ya kuugua kwake na kupona:
10 Nilisema, “Katika ustawi wa maisha yangu,
je, ni lazima nipite katika malango ya mauti,*
na kupokonywa miaka yangu iliyobaki?”
11 Nilisema, “Sitamwona tena Bwana,
Bwana katika nchi ya walio hai,
wala sitamtazama tena mwanadamu,
wala kuwa na wale ambao sasa wanakaa katika ulimwengu huu.
12 Kama hema la mchunga mifugo,
nyumba yangu imebomolewa na kutwaliwa kutoka kwangu.
Kama mfumaji nimevingirisha maisha yangu,
naye amenikatilia mbali kutoka kitanda cha mfumi.
Mchana na usiku uliyakomesha maisha yangu.
13 Nilingoja kwa uvumilivu hadi mapambazuko,
lakini alivunja mifupa yangu yote kama simba.
Mchana na usiku uliyakomesha maisha yangu.
14 Nililia kama mbayuwayu au korongo,
niliomboleza kama hua aombolezaye.
Macho yangu yalififia nilipotazama mbinguni.
Ee Bwana, ninataabika, njoo unisaidie!”
 
15 Lakini niseme nini?
Amesema nami, naye yeye mwenyewe amelitenda hili.
Nitatembea kwa unyenyekevu
katika miaka yangu yote
kwa sababu ya haya maumivu makali
ya nafsi yangu.
16 Bwana, kwa mambo kama haya watu huishi,
nayo roho yangu hupata uzima katika hayo pia.
Uliniponya
na kuniacha niishi.
17 Hakika ilikuwa ya faida yangu
ndiyo maana nikapata maumivu makali.
Katika upendo wako ukaniokoa
kutoka shimo la uharibifu;
umeziweka dhambi zangu zote
nyuma yako.
18 Kwa maana kaburi haliwezi kukusifu,
mauti haiwezi kuimba sifa zako;
wale washukao chini shimoni
hawawezi kuutarajia uaminifu wako.
19 Walio hai, walio hai: hao wanakusifu,
kama ninavyofanya leo.
Baba huwaambia watoto wao
habari za uaminifu wako.
 
20 Bwana ataniokoa,
nasi tutaimba kwa vyombo vya nyuzi
siku zote za maisha yetu
katika Hekalu la Bwana.
21 Isaya alikuwa amesema, “Tengenezeni dawa ya kubandika ya tini, mweke juu ya jipu, naye atapona.”
22 Hezekia alikuwa ameuliza, “Kutakuwa na ishara gani kwamba nitapanda kwenda Hekalu la Bwana?”
* 38:10 Mauti hapa maana yake ni Kuzimu. 38:18 Kaburini hapa maana yake ni Kuzimu, kwa Kiebrania ni Sheol.