39
Wajumbe Kutoka Babeli
(2 Wafalme 20:12-19)
Wakati huo Merodaki-Baladani, mwana wa Baladani mfalme wa Babeli, akamtumia Hezekia barua na zawadi, kwa sababu alikuwa amesikia habari za kuugua na kupona kwake. Hezekia akawapokea wale wajumbe kwa furaha na kuwaonyesha vitu vile vilivyokuwa katika ghala zake: yaani fedha, dhahabu, vikolezo na mafuta safi, ghala la silaha lote, na kila kitu kilichokuwa katika hazina zake. Hapakuwa na kitu chochote katika jumba lake la kifalme au katika ufalme wake wote ambacho Hezekia hakuwaonyesha.
Ndipo nabii Isaya akaenda kwa Mfalme Hezekia na kumuuliza, “Watu hao walisema nini, na wametoka wapi?”
Hezekia akamjibu, “Wametoka nchi ya mbali. Walikuja kwangu kutoka Babeli.”
Nabii akauliza, “Waliona nini katika jumba lako la kifalme?”
Hezekia akajibu, “Waliona kila kitu katika jumba langu la kifalme. Hakuna kitu chochote katika hazina yangu ambacho sikuwaonyesha.”
Ndipo Isaya akamwambia Hezekia, “Sikia neno la Bwana Mwenye Nguvu Zote: Hakika wakati unakuja ambapo vitu vyote katika jumba lako la kifalme, na vyote ambavyo baba zako waliweka akiba mpaka siku hii, vitachukuliwa kwenda Babeli. Hakuna chochote kitakachosalia, asema Bwana. Nao baadhi ya wazao wako, nyama yako na damu yako mwenyewe watakaozaliwa kwako, watachukuliwa mbali, nao watakuwa matowashi katika jumba la mfalme wa Babeli.”
Hezekia akamjibu Isaya, “Neno la Bwana ulilosema ni jema.” Kwa kuwa alifikiri, “Patakuwepo amani na usalama wakati wa uhai wangu.”